NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa hawachukulii wapinzani kama maadui bali anawachukulia kuwa ni watu wanamuonyesha changamoto ili aweze kuzitatua.
Rais Samia ameyasema hayo leo Machi 5, 2023 wakati akisalimiana na wananchi wa USA River jijini Arusha ambapo amesema mtanzania yeyote awe chama chochote cha siasa kinachotofautisha ni mawazo na fikra tu.
Amesisitiza kuwa yeye awachukulii wapinzani kama maadui bali kama watu watakaomuonesha changamoto zilizopo azitekeleze ili Chama cha Mapinduzi (CCM) kiimarike.
“Kwahiyo mdogo wangu (Lema) amerudi, aliniambia mama nataka kurudi, nikamwambia rudi, akasema mama nina kesi, nikawambia nina kesi nikamwambia nazifuta rudi, amerudi tuimarishe siasa si ndio.
“Mwanaume ni yule anayejiamini, mwanamke ni yule anayejiamini, kwahiyo kwenye uwanja wa siasa tunajiamini tupo vizuri na tutakwenda vizuri, nawashukuru watoto wangu wa bodaboda wamenisindikiza toka mjini mpaka hapa, mwendo ni huohuo hadi 2025, nawatambua,” amesema Rais Samia
Aidha amesema watashughulika na kupeleka fedha kwenye maendeleo ya wananchi na kwamba hawatayakata maeneo ya utawala kwani yakikatwa yataongeza gharama kwenye utawala na kunyima fedha kwenda kwa wananchi kwenye maji elimu, umeme au kutoa ruzuku ya mbolea.
“Fedha hizi zitatumika kuhudumia wananchi hivyo kwasasa serikali haitakata maeneo ya utawala. Aidha nawahakikisia kuwa kwenye uchumi tupo vizuri, kwenye maendeleo ya watu tupo vizuri, tunajitahidi sana kuimarisha miundombinu ya maeneo ili wananchi wapate huduma kwa karibu zaidi,” amesema