NA MWANDISHI WETU, MWANZA
JESHI la polisi Mkoani Mwanza linawashikilia watu 18 kwa tuhuma mbalimbali wakiwemo walimu wanane wa shule za Msingi kwa tuhuma za kuiba zaidi ya Sh.Mil.273 /-kutoka Benki ya Walimu (MCB) kwa njia ya mtandao.
Kamanda Mutafungwa amewaambia waandishi habari jijini Mwanza Machi 3, 2023 kuwa walimu hao wanaotoka shule tofauti wanadaiwa kufanya wizi huo Februari 20, mwaka huu kwa kujihamishia fedha kwenye akaunti zao baada ya kuingilia mawasiliano na mfumo wa benki.
Amewataja wanaoshikiliwa na shule wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Gasper Maganga (shule ya msingi Kilabela) Wilaya ya Sengerema, Marwa Mwita (shule ya msingi Nyitundu Sengerema), Masaba Mnanka (Shule ya Msingi Kilabela), Harold Madia (Bugumbikiswa), Clever Banda (Sekondari ya Nyamatongo Sengerema), Justin Ndiege (Shule ya Msingi Ishishangolo), Fredrick Ndiege (Pamba C) na Steven Sambali anayetoka shule ya msingi Nyangongwa.
“Katika upekuzi, baadhi ya watuhumiwa hao wamekutwa na fedha tasilimu na mali ikiwemo pikipiki inayodaiwa kununuliwa kwa fedha za wizi,” amesema Kamanda Mutafungwa.
Katika tukio jingine, Kamanda Mutafungwa amesema jeshi hilo linamshikilia George Shaban (55) mkazi wa Mahina Jijini Mwanza kwa tuhuma za kumuua kwa kipigo mtoto wake, Emmanuel Shaban (14), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyangulugulu.
Baba huyo aliyejisalimisha mwenyewe Kituo cha Polisi anadaiwa kumshushia kipigo mtoto wake baada ya kupokea malalamiko kuwa alikwanyua mahindi mabichi mawili kutoka kwenye shamba la jirani yao ambaye hakutajwa jina.
Jeshi la Polisi pia linawashikiliwa watu wengine wanne kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha Pius Makoye, mlinzi wa Kituo cha Mafuta cha Bulunda Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kilichotokea Januari 8, mwaka huu.
Katika tukio hilo, watuhumiwa hao wanadaiwa kumshambulia mlinzi huyo sehemu mbalimbali ya mwili kwa na kufanikiwa kupora Sh.milioni 3.8/-
Kamanda Mutafungwa amesema Jeshi hilo pia linamshikilia Jerry Mjele (31), mkulima mkazi wa Bunda mkoani Mara kwa tuhuma za kumuua Chuma Geradi (27), mkazi wa Kijiji cha Kayula Wilaya ya Sengerema katika tukio lililotokea Machi 2, 2023 baada ya ugomvi uliotokea kwenye kilabu ya pombe.
Jeshi hilo pia limefanikiwa kumtia mbaroni Lucas Musa (24), mkazi wa Mtaa Mbege eneo la Mkolani aliyekuwa akisakwa kwa tuhuma za kuhusika kwenye matukio kadhaa ya kihalifu likiwemo kuvamia na kuvunja nyumba Josephine Leonard lililotokea Februari 21, mwaka huu mtaa wa Kahama wilayani Ilemela.
Mtuhumiwa anadaiwa kukutwa na mali kadhaa zinazoaminika kuwa za wizi ikiwemo seti mbili za Runinga, sabufa mbili, kompyuta na vifaa vya kuvunjia milango.
Mtuhumiwa mwingine anayeshikiliwa na Polisi ni Prisca Lameck, mkazi wa Nyakato anayedaiwa kumtupa mtoto wake mwenye umri wa miezi mitatu ambaye hata hivyo aliokolewa na msamaria mwema. Tukio hilo lilitokea Februari 20, 2023.