NA MWANDISHI WETU,SINGIDA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Singida imemuhukumu adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha jela mkazi wa Manispaa ya Singida Fabiano Darabe (50)baada ya kumtia hatiani kwa jumla ya makosa matano ya kubaka na kulawiti.
Mwanasheria wa serikali,Nuru Chiwalo alidai katika Mahakama hiyo kwamba mtuhumiwa alitenda makosa mawili ya ubakaji na makosa matatu ya ulawiti kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka mitano na miaka 11 katika Manispaa ya Singida kwa kipindi cha kati ya mwaka 2018 hadi mwaka 2021.
‘’Mtuhumiwa alitenda kosa la kubaka mwanafunzi wa darasa la tano mwenye umri wa miaka 11 na kumlawiti mwanafunzi wa darasa la pili mwenye umri wa miaka saba,vile vile alimlawiti mwanafunzi wa darasa la kwanza wakati akijua wazi kuwa kutenda kosa hilo ni kinyume cha sheria za nchi’’alisisitiza Mwanasheria huyo wa serikali.
Kwa mujibu wa Chiwalo serikali iliwasilisha mashahidi wanane ambao walitoa ushahidi wa vielelezo ikiwemo PF3,mlinzi wa amani,Deodatus Patrick na daktari ambaye alithibitisha kwamba watoto hao walifanyiwa vitendo hivyo vya ukatili.
Kabla ya Hakimu wa Mahakama hiyo kumtia hatiani mtuhumiwa,Mwanasheria wa serikali alidai kwamba matukio ya vitendo vya ubakaji na ulawiti katika Mkoa wa Singida yamekithiri mbele ya jamii na kwamba vitendo hivyo vinasababisha watu kuwa mashoga.
Hata hivyo , Chiwalo alidai kuwa Mahakama hiyo haina kumbu kumbu za makosa mengine ya nyuma ya mtuhumiwa huyo lakini hata hivyo aliiomba Mahakama hiyo kuangalia sheria inasema nini kwa wakosaji wa makosa ya aina hiyo kwani kitenndo cha mtoto kuingiliwa kunazuia mtoto huyo kupata haja kubwa.
‘’Adhabu utakayotoa ilenge kutoa elimu kwa jamii kuachana na tabia ya kuwabaka au kuwalati watoto wadogo na adhabu hiyo iwe fundisho kwa wazazi na walezi wengine ambao bado hawajajulikana kuwa wanajihusisha na vitendo vya aina hii.’’alisisitiza Chiwalo.
Alipotakiwa kutoa utetezi wake baada ya Mahakama kumtia hatiani ni kwa nini asipewe adhabu kali,Darabe aliiomba Mahakama impungizie adhabu kwa kuwa ana matatizo ya kiafya.
‘’Lakini Mheshimiwa Hakimu acha tu nikafie huko huko tu si wameamua kunileta huku kwa kosa ambalo sikulitenda kabisa mimi mwenyewe.’’alisikika akiiomba Mahakama hiyo kwa sauti ya chini huku akimtazama Hakimu kabla ya kutoa hukumu yake.
Hakimu wa Mahakama hiyo Robert Oguda alisema vitendo vya ubakaji wa watoto chini ya miaka kumi adhabu yake ni kifungo cha maisha na kuanzia miaka 11 adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.
Akitoa hukumu ya mashitaka hayo matano,Hakimu Oguda alisema kwa kosa la kwanza na kosa la tatu mtuhumiwa atakwenda kutumikia adhabu ya miaka 30 jela kwa kila kosa na kwamba kwa kosa la pili,la nne na la tano mtuhumiwa atakwenda kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Hata hivyo Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo aliweka bayana kwamba kwa ujumla adhabu za makosa hayo yota yataenda kwa pamoja,hivyo mshitakiwa huyo atatumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela.