NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk.Hussein Mwinyi, ametoa maagizo kwa taasisi zilizo chini ya serikali hiyo zikiwemo za afya kutengeneza sera ambazo zitatoa uhakika wa matibabu bila kikwazo kwa watoto wanaougua magonjwa adimu.
Dk.Mwinyi alitoa kauli hiyo juzi wakati wa maadhimisho ya siku ya magonjwa adimu yaliyofanyika katika Hospitali ya Aghakhan jijini Dar es Salaam kwa kuwasha taa kama ishara ya kuitambua siku hiyo.
“Mimi na serikali yangu nataka niseme kwamba kwanza suala hili tunalitambua na tutafanya kila litakalowezekana kutoa mchango wetu katika kushughulikia watoto walioathirika na magonjwa haya,”alisema na kuongeza kuwa
“Nadhani sasa hivi kinachotakiwa ni kuendelea kutoa elimu kwa umma ili utambue kwamba kuna watoto walioathirika na ugonjwa huo na wanahitaji msaada kwa maisha yao yote, lakini nazitaka taasisi za umma kutambua kuwapo kwa ugonjwa huo na kutengeneza sera za kuutambua”
Kwa upande wake, Sharifa Mbarak, Mama mwenye mtoto aishiye na magonjwa adimu alisema licha serikali kuendelea kuweka mipango mizuri kwa watoto hao lakini bado wamekuwa wanapata shida upande wa sekta ya afya.
Alisema asilimia kubwa ya watoto hao wanapoumwa wanaingia katika gharama kubwa kutokana na matibabu yao ufanywa katika hospitali kubwa na sio ndogo ndogo kutokana na vifaa vya vipimo kutokuwepo katika hospitali hizo ndogo.
Sharifa alieleza kuwa, watoto hao hutakiwa kutumia mashine za kupumulia na kuongezewa Oksijeni muda wote kwa baadhi yao ambapo upatikanaji wa oksijeni una urasimu mkubwa na sio kila mtu ataweza kulipia gharama hiyo.
Naye Daktari wa Watoto Hospitali ya Aghakhan, Mariam Nooran, alisema ugonjwa huo huwapata wachache na hutokana na kurithi kutoka kwenye vinasaba.
Sarah Chande, ambaye ni mke wa Mchora Katuni , Masoud Kipanya, alisema yeye amewahi kuishi na mtoto mwenye ugonjwa huo na kwamba gharama ya matibabu kwa magonjwa hayo ni kubwa pamoja na huduma za kila siku ambazo huhitaji.