NA MWANDISHI WETU, DODOMA
MAHAKAMA Kuu kanda ya Dodoma imesema itatoa amri za msingi katika kesi ya maombi madogo namba 17/2022 iliyofunguliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha walimu Tanzania (CWT), Deus Seif na mweka hazina, Abubakar Alawi ifikapo Machi 13, 2023.
Katika maombi hayo, Deus na mwenzake wameiomba Mahakama iuchukulie hatua uongozi wa chama hicho kwa kukiuka amri halali ya Mahakama iliyozuia kujadili ajenda ya shauri la kinidhamu dhidi yao kwenye mkutano uliofanyika Desemba 15 na 16, 2022.
Akizungumza leo Februari 28, nje ya Mahakama hiyo wakili wa upande wa walalamikaji, Jeremiah Mtobesya amesema Mahakama ilitoa amri hiyo Desemba 13, 2022 kutokana na viongozi hao kuwa na mashauri ya jinai Mahakama ya rufaa.
Hata hivyo, Mtobesya amesema Desemba 14, 2022 upande wa CWT waliwafikishia amri hiyo na ilipokelewa, lakini katika mkutano huo waliendelea kujadili masuala hayo ambayo Mahakama iliyazuia.
Akijibu hoja za ukiukwaji wa amri ya Mahakama kuhusu kujadili ajenda hiyo wakili wa upande wa CWT, Leonard Haule amedai kusikitishwa kuwa amri ya Mahakama ya kuzuia ajenda hiyo ilikwenda kwenye uongozi wa chama hicho wakati mkutano ukiwa umeshafanyika yaani Desemba 17, 2022.
Haule amesema mtu wa masijala aliyepokea na kusaini amri hiyo aliipeleka barua hiyo kwa uongozi wa chama baada ya mkutano kuisha kwa kudhani kuwa ilikuwa ni nyaraka ya kawaida.
“Baada ya kusoma ule uamuzi na kuona kuna file limefunguliwa Mahakamani kwa muda wa kutosha na amri zimetolewa lakini kwa makusudi hawakuweza kupeleka nakala kwenye uongozi wa CWT ambao upo hapo karibu na Mahakama ndipo niliamua kufatilia,” amedai Haule.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Jaji anayesikiliza kesi hiyo Adam Mambi amesema Mahakama itatoa amri za msingi juu ya maombi hayo madogo na kuendelea kutajwa kwa kesi ya msingi namba 18, 2022.