NA MWANDISHI WETU DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha uhifadhi, kuongeza idadi ya watalii na kukuza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa, huku likilenga kuongeza manufaa ya wananchi wanaozunguka hifadhi.
Akizungumza katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam leo Jumanne Novemba 10, 2026,Kamishna Masssana Mwishawa amesema Serikali imeboresha miundombinu ya kufikia hifadhi kupitia ujenzi wa viwanja vinne vya ndege katika Hifadhi za Nyerere, Mikumi na Ruaha, uwekezaji katika reli ya kisasa ya SGR na uboreshaji wa barabara.
Amesema TANAPA pia imeimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika doria, ufuatiliaji wa wanyamapori na kudhibiti ujangili, huku wananchi wakipewa namba maalumu za kutoa taarifa kuhusu wanyamapori wakali na waharibifu.
Aidha Kamishna Mwishawa amesema Katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, shirika hilo linaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, mabweni, zahanati, vituo vya polisi, visima na mabwawa ya maji.
Pia amesema ,imewezesha vikundi vya wananchi kupitia benki za jamii za COCOBA na miradi ya uchakataji wa asali na mafuta ya alizeti.
Aidha,amesema TANAPA imewekeza katika kukuza utalii wa michezo kupitia uwanja wa gofu wa Fort Ikoma, karibu na Hifadhi ya Taifa Serengeti, unaolenga kuvutia watalii wa kimataifa na kuongeza fursa za uwekezaji.
Katika mkakati mwingine,Kamishna Mwishawa amebainisha kuwa TANAPA kwa kushirikiana na wadau wa utalii imepanga kuandaa vifurushi maalumu vya utalii wakati wa mashindano ya AFCON, vitakavyowawezesha mashabiki kutembelea hifadhi za Serengeti, Nyerere, Saadani, Mikumi, Tarangire, Arusha na Manyara.
“Mikakati mingine ni ujenzi wa barabara ya kilomita 6.69 kutoka lango kuu la Hifadhi ya Manyara hadi Minjingu na kuanzisha utalii wa majini katika Ziwa Victoria, utakaounganisha Serengeti, Kisiwa cha Saanane, Rubondo na Burigi-Chato.” amefafanua
Pamoja na mambo mengine,
Kamishna Mwishawa amewataka wahariri na waandishi wa habari kushirikiana na TANAPA kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi, huku wananchi wakihimizwa kulinda rasilimali za hifadhi na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na utalii.

