NA JOSEPH MAHUMI,WF,THAILAND
WAZIRI wa Fedha,Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewasili jijini Bangkok nchini Thailand, ambapo ataongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika nchini humo kuanzia Oktoba 12 hadi 18,2026.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Suvarnabhumi, Balozi Omar, aliyeambatana na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Dk. Juma Malik Akil, alilakiwa na Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini Thailand, Florean Rwehumbiza pamoja na Naibu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Kaimu Mshauri Mkuu wa Usimamizi na Uendelezaji wa Ukusanyaji wa Mapato wa Thailand,Yutuna Phoolpipat.
Balozi Omar ni Gavana anayewakilisha Tanzania katika Shirika la IMF na Benki ya Dunia, ambayo Tanzania ni nchi mwanachama.
Taasisi hizo za fedha ni wadau muhimu katika kusaidia juhudi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kupitia ushirikiano wa kifedha, kiufundi na kisera.




