NA MWANDISHI WETU,LONDON,UINGEREZA
WAZIRI MKUU Dk. Mwigulu Nchemba amesema ni muhimu kuendelea kuweka katika matumizi ya teknolojia itakayowezesha nchi kuongeza thamani ya madini adimu (critical minerals) badala ya kuyauza katika hali ghafi.
Amesema hayo leo (Jumatano, Oktoba 7, 2026) wakati akipokea taarifa ya Utafiti ya uongezaji thamani na uchimbaji wa madini adimu iliyofanywa na wataalamu wa kampuni ya McKinsey ya Uingereza katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Hyatt, jijini London, Uingereza.
Kikao hicho kimejadili matokeo ya utafiti huo, pamoja na fursa zinazoweza kutumiwa na Tanzania katika kuongeza thamani ya madini adimu nchini badala ya kuyauza katika hali ghafi. Aidha, wameangalia umuhimu wa matumizia ya teknolojia, uwekezaji na utaalamu katika kujenga uwezo wa ndani wa kuchakata na kuzalisha bidhaa zitokanazo na madini hayo.
Dk.Nchemba amesisitiza umuhimu wa Tanzania kutumia rasilimali zake za madini adhimu kama kichocheo cha uchumi na maendeleo ya viwanda, kwa kuweka mazingira wezeshi yatakayovutia uwekezaji na kuongeza manufaa kwa Taifa.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika tafiti, ubunifu na uwekezaji katika sekta ya madini ili kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kuongeza thamani, kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa Tanzania.


