NA BARAKA JUMA, Mwanza
MWANAMKE mmoja mkazi wa kata ya Maisome, Buchosa, wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Edyner Metodi (34) ameuawa kwa kuliwa na Mamba wakati alipokuwa akioga ziwa Victoria.
Akithibisha kuwepo kwa tukio hilo mkuu wa wilaya ya Sengerema Senyi Ngaga alisema tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati mwanamke huyo alipokuwa akioga na watoto wake wawili na pamoja na mwanamke mmoja ambao hawakutajwa majina na ndio waliousika kutoa taarifa kwenye eneo la uongozi wa kijiji kuhusu tukio hilo.
“Baada tu yakupata taarifa tulianza taratibu za kuusaka mwili huo ziwa Victoria kwa kushirikiana na watu wa zima moto na uokowaji na ndipo tulibahatika kupata mabaki ya mwili huo. Nitoe wito kwa wananchi wote waache tabia ya kuecheza na kuoga ziwani na badala yake wachote maji wakaogee nyumbani, alisema Ngaga.
Kwa upande wake, diwani wa kata ya Maisome, Damson Katama alisema matukio ya Mamba kula wananchi wake yamekithiri kwenye eneo lake na ameshalalamika kwa idara zinazousika na wanyamapori na hakuna hatuwa zozote zilizochukuliwa dhidi ya wanyama hao hatari.
“Kama wameshindwa kuwauwa hawa Mamba wanaokula watu waturuhusu sisi tuwauwe kwasababu matukio ya Mamba kula wananchi wangu yamekithiri sana”, alisema Katama.
Naye, Mgane wa marehemu, Mohammed Kisanyenge alisema matatizo kama hayo kwenye vijiji vingine yameshatokea na wao kama familia wamelipokea kwa masikitiko makubwa na marehemu ameacha watoto sita kati yao wakiume watatu na wakike watatu.
Katika hatua nyingine alipotafutwa kwa simu kwa nyakati tofauti kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Wilbrod Mtafungwa simu yake iliita pasipo kupokelewa.
Nao, baadhi ya wananchi wa eneo hilo ambao hakuwa tayali kutajwa majina yao gazetini waliilalamikia serikali kuu kwa kutosikia kilio chao hicho cha muda mrefu na kudai matukio kama hayo yamekuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari hapa nchini mara kwa mara rakini hakuna hatuwa zilizochukuliwa.