Na ANTHONY SOLO, DODOMA.
BODI ya Maji Bonde la Wami-Ruvu imewataka wadau wa maji nchini kufuata taratibu za uchimbaji wa visima vya maji ikiwemo kuomba vibali ili kupata maji yenye ubora yatakayoondoa malalamiko mengi kuhusu maji yasiyo na viwango.
Akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami – Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi, Februari 7, 2023 alisema ili kuondokana na malalamiko ya maji kukosa viwango wadau hawana budi kuomba vibali kabla ya kuchimba visima holela.
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji chini ya bodi hiyo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa wadau wa maji wanapaswa kufahamu madhara ya kuchimba visima bila vibali jambo ambalo linapelekea changamoto ya ubora wa maji kwenye maeneo mengi.
Aidha Mkurugenzi huyo alieleza baadhi ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kupata maji yasiyo na madhara ambapo hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha maji yanayopatikana baada ya kuchimbwa yanapelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi kubaini kama yanafaa kwa matumizi au la.
Sambamba na hayo Mkurugenzi Mmasi alisema kuwa bodi hiyo imejipanga kuhakikisha inamaliza changamoto ya tatizo la maji katika Mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro kwa kuchimba visima 10 vyenye maji ya kutosha.
“Bodi hiyo pia imejipanga kuhakikisha inaondoa tatizo la maji katika mikoa ambayo imekuwa na changamoto ya maji hususani katika mkoa wa Pwani, Morogoro na Dar es salaam”alisema Mmasi.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Bodi ya maji alisema Bodi hiyo imefanikiwa kubaini vyanzo vipya vya maji ambavyo ni eneo la Nzuguni lililopo Jijini Dodoma ambalo linaonekana lina maji ya kutosha.
“Hivi karibuni tutalitangaza eneo la Nzuguni katika mji wa Dodoma pamoja na Dakawa katika gazeti la Serikali kuwa maeneo hayo ni benki ya maji”amesema.
Kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji Mkurugenzi Mmasi alisema watahakikisha vyanzo vyote vinatunzwa kwa ajili ya kutunza maji yaliyopo chini ya Ardhi huku akiwataka watanzania kuepukana na tabia ya uchimbaji holela wa visima vya maji.
Mmasi alisema kuwa kuwa uchimbaji holela wa visima unaweza kusababisha kuchafua maji yaliyopo chini ya ardhi jambo ambalo ni hatari kwani liweza kuzuia namnan ya kuondoa sumu.
Akihitimisha Mkurugenzi huyo alisema mikakati ya Bodi hiyo ni kuhakikisha Bonde hilo linakuwa kwenye Mazingira safi na kijani linalotunza na kuendeleza vyanzo vya maji kwa maendeleo ya Binadamu kijamii na kiuchumi yanayostahimili majanga yanayoweza kutokea kutokana na maji.