Na MWANDISHI WETU
WAUMINI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam, wameshukuru kwa hatua ya msamaha aliopewa Mchungaji Dk Eliona Kimaro, baada ya kutumikia likizo ya lazima kwa siku 35 kati ya siku 60 alizopewa kwa kuwa inaleta amani katika Kanisa.
Wakizungumza na Demokrasia jana, waumini hao walieleza kuwa wanaamini msamaha huo umetolewa kimkakati ili kulinusuru Kanisa na Usharika wa Kijitonyama, kwa kuwa msukumo wa kutaka kujua makosa aliyofanya mchungaji huyo uliibua na kuanika mambo mengi ambayo yalijificha.
Mmoja wa waumini, Arcado Mutta alisema pamoja na kuomba msamaha, inaonekana mchungaji huyo alisukumwa na uongozi ili kujaribu kunusuri heshima yao na ya Kanisa, baada ya kuona mwenendo wa tuhuma dhidi yake ukiliyumbisha Kanisa.
“Ni kawaida, mama au baba yako akikuadhibu bila kosa, wazee watakwambia omba msamaha hata kana huna kosa. Hili ni suala lililoandaliw ana kuratibiwa, ndiyo maana wamemuita kusali huko na kuandaa taratibu za kumtaka aombe msamaha hata kama anaona hana kosa, ili kuwanusuru viongozi kwa kuwa walishaona walipokosea, hicho ndicho kilichotokea,” alisema.
Msharika mwingine, Aniceth Shayo alisema hatua hiyo imefanyika makusudi ili kunusuru mapato ambayo tayari yalishaanza kuyumba, lakini pia kuusafisha uongozi wa Dayosisi ambao pia ulishaanza kuyumba kutokana na uongozi huo.
Msharika mwingine, Mercy Kibabu alisema ni jambo la kufurahisha na kuleta amani baada ya hatua ya uongozi wa Dayosisi kuamua kumfutia adhabu hiyo na kumsamehe Mchungaji Dk Kimaro, kwa kuwa busara iliyotumika inaonesha wazi Roho Mtakatifu amekuwa upande wao.
Kauli hizo zimetolewa muda mfupi baada ya Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa kutangaza msamaha kwa Mchungaji wa Ushirika wa Kijitonyama, Dk Eliona Kimaro jana, ambaye alipewa likizo ya siku 60.
Dk Malasusa alitangaza msamaha huo ikiwa ni siku 35 tangu alipopewa likizo ya siku 60 kama adhabu, kwa makosa ambayo hayakuwekwa hadharani, hatua inayomfanya kurudi kazini ikiwa bado siku 25 kumaliza adhabu hiyo.
Akitangaza msamaha kwa Mchungaji Dk Kimaro jana, akiwa kwenye Ibada iliyofanyika Ushirika wa Kinyerezi jana, Februari 19, Askofu Dk Malasusa ambaye ndiye aliyeongoza ibada hiyo alisema ametangaza uamuzi huo Kanisani baada ya Mchungaji Kimaro kupewa fursa ya kuwasalimia waumini na akaomba radhi kwa yote yaliyotokea.
“…Mchungaji Kimaro kama ulivyoomba umesamehewa, endelea kutafakari, endelea kukaa karibu na Mungu wako,” alisema Askofu Dk Malasusa huku akiwaomba waumini washirika mbalimbali kuwatunza na kuwaombea wachungaji wao.
Awali, akizungumza baada ya kupewa nafasi ya kuomba msamaha mbele ya washarika, Mchungaji Dk Kimaro alisema anatumia fursa hiyo kwa moyo wa unyenyekevu na anajisikia kunyenyekea ndani ya moyo wake, kuomba radhi na msamaha kwa askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Malasusa, kwa ajili ya mambo mengi yaliyoendelea na yaliyosikika kwenye mitandao na mengine hayakuwa na sura nzuri.
“Askofu Dk Malasusa nikushukuru sana kwa uvumilivu wako. Tarehe 13/11 mwaka jana, ilikuwa siku yetu ya mavuno katika Usgarika wa Kijitonyama, niliongoza ibada na semina fupi na kuwaombea wanafunzi wa kidato cha nne, na mwishoni kabisa mwa ibada nilisukumwa kuwaombea vijana wasio na ajira ili waweze kujiajiri peke yao.
“Katika kuwaombea wale vijana nilisisitiza suala la uaminifu, nidhamu ya maisha na nidhamu binafsi. Katika kusisitiza nilitoa mfano wa vijana wa kikristo wa usharika wangu wa Kijitonyama na wa dhehebu jingine lakini pengine nitamke hapa wazi, wale vijana wa Kiislamu.
“Baada ya hapo maneno yale yalisambaa huko duniani na ikatengeneza kipande cha video kilichoonesha ulinganifu kati ya waislamu na wakristo katika suala la uaminifu, hasa vijana. Jambo hilo limeleta mtafaruku miubw akatika jamii na limeleta sintofahamu, kina ambao wamepokea vyema na ambao wamepokea tofauti,” alisema.
Alisema maamuzi ya Askofu Dk Malasusa ambaye pia umekuwa mkuu wa KKKT kwa miaka 10, ameheshimiwa na Kanisa na maamuzi yake ni maamuzi ya busara na yeye anayapokea kwa moyo wa unyenyekevu kama mchungaji mwenye kiapo na nadhiri za daima za uchungaji, kutii maelekezo ya Askofu.
“Katika utaratibu wa Kanisa, Nidhamu ya Kanisa na agizo la Kanisa kuna mambo ambayo lazima viongozi wa Kanisa wayachukue na moja ya mambo ya msingi waliyokua ni pamoja na kupata mapumziko ya kutafakari na moja kwa moja nimekwenda kwenye mapumziko kwenye nyumba za malezi ya kichungani na ndiko nilikotokea,” alisema.
Akiwa katika ibada ya maombi na semina kwenye Usharika wa Kijitonyama (KKKT), usiku wa Januari 16, 2023 Mchungaji Dk Kimaro alionekana kupitia video iliyosambazwa kwa waumini na kweye mitandao ya kijamii, akiwaaga kwa machozi kwa kile alichoeleza kuwa amepokea barua kutoka kwa msaidizi wa Akofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani kwamba amepokea baria ikimtaka kwenda likizo ya siku 60 na akirejea akaripoti makao makuu ya Dayosisi.
Alieleza kuwa amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa katika ofisi ya msaidizi wa Askofu na kufanya kikao na mkuu wa jimbo.
Likizo hiyo ilikuwa inamalizika Machi 17, 2023 na Mchungaji Kimaro alipokuwa akiwaaga Washirika wa Kijitonyama alisema baada ya likizo hiyo hatarudi hapo, alielezwa akaripoti Makao Makuu ya Dayosisi.
Mchungaji Dk Kimaro ameomba radhi kwa Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Fredrick Shoo kwa usumbufu wowote uliojitokeza wakati huu ambao amekuwa likizo.
“Naomba radhi kwa mkuu wa kanisa Askofu, Dk Fredrick Shoo kwa usumbufu wowote ambao ulijitokeza katika mitandao na kwenye vyombo vya habari kwa wakati huu ambao nimekuwa likizo ya faragha,” alisema Dk Kimaro.