NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KITABU kinachoelezea falsafa ya sheria ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan,
kimeelezwa kuwa kinaweka mtazamo mpya unaoonesha kuwa sheria si chombo cha kusimamia Mahakama na vyombo vya dola pekee, bali ni msingi muhimu wa maendeleo ya uchumi, ujenzi wa taasisi imara na ustawi wa jamii.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah alipomuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, katika Uzinduzi wa Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia uliofanyika katika Ukumbi wa Maktaba mpya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Julai 10, 2026.
Alisema kazi hiyo ya kitaaluma inawapa wananchi nafasi ya kutafakari kwa kina falsafa ya uongozi wa Rais Samia tangu alipoingia madarakani mwezi Machi mwaka 2021, akisisitiza maridhiano, mageuzi, ustahimilivu, ujenzi wa taasisi, ukuaji wa uchumi na kuvutia uwekezaji.
Abdullah alisema kitabu hicho kinafafanua kwa uchambuzi wa kisheria jinsi mageuzi yanavyopaswa kuanzia katika utambuzi wa changamoto za sera na sheria, kufuatiwa na kuimarishwa kwa taasisi, matumizi ya teknolojia na rasilimali watu, kabla ya matokeo yake kuonekana katika maisha ya wananchi.
Makamu huyo alieleza kuwa sheria nzuri haziwezi kuleta matokeo endapo hazitasimamiwa na taasisi imara zenye uwazi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya teknolojia, akisisitiza kuwa mageuzi yanapaswa kuangaliwa kama mfumo mzima badala ya tukio la wakati mmoja.
Aidha, alisema kitabu hicho kimegawanywa katika sehemu tatu zinazojadili misingi ya kifalsafa ya sheria, mageuzi ya uchumi na uwekezaji pamoja na masuala ya demokrasia, msaada wa kisheria, usawa wa kijinsia na mwelekeo wa maendeleo ya baadaye.
Akizungumzia mafanikio yaliyoainishwa katika kitabu hicho, alisema mapato ya ndani ya Serikali yameongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, hatua ambayo imeongeza uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, reli, umeme, maji na huduma za afya kupitia rasilimali za ndani.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa ongezeko la mapato linapaswa kuendana na mfumo wa kodi ulio rafiki na unaochochea ukuaji wa sekta binafsi.
Pia alisema mageuzi ya mfumo wa kodi yanapaswa kuzingatia mabadiliko ya uchumi wa kidijitali, biashara za mtandaoni na mifumo ya malipo ya kielektroniki ili kuhakikisha Serikali inaendelea kukusanya mapato bila kuathiri ubunifu wa vijana na ukuaji wa biashara ndogo na za kati.
Kwa upande wa uwekezaji, alisema maboresho ya sheria za uwekezaji na hatua za kurahisisha utoaji wa huduma kwa wawekezaji yameweka mazingira bora zaidi ya biashara kwa kupunguza urasimu na kuongeza uwazi katika utoaji wa vibali na huduma nyingine muhimu.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inalenga kuvutia uwekezaji wenye tija utakaoongeza ajira, kuhamisha teknolojia, kuongeza mapato ya Serikali na kukuza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za uchumi.
Alitoa wito kwa wasomi, wataalamu wa sheria na watunga sera kuendelea kutumia kitabu hicho kama rejea muhimu katika kujenga mifumo ya sheria inayochochea maendeleo jumuishi, kulinda haki za wananchi na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema kitabu cha “Falsafa ya Sheria ya Mama Samia” kimeandaliwa kwa lengo la kuonyesha jinsi sheria ilivyotumika kama nyenzo ya kuleta mageuzi, maendeleo na kuimarisha utawala bora chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema sheria ndiyo msingi wa uwajibikaji, usimamizi wa rasilimali, ulinzi wa haki za wananchi na ujenzi wa taasisi imara zinazochochea maendeleo ya taifa.
Alitoa shukrani kwa Wizara ya Katiba na Sheria, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chama cha Mawakili wa Serikali, waandishi, wahakiki, wahariri na wadau wote walioshiriki kufanikisha uandishi wa kitabu hicho.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba, amesema utawala wa sheria, haki, usawa mbele ya sheria na ulinzi wa haki za binadamu ni nguzo muhimu zinazochochea maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini.
Katimba alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha misingi hiyo kupitia maboresho ya sheria, sera na mifumo mbalimbali ya utoaji wa haki.
Alisisitza pia Serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, huku ikiongeza upatikanaji wa elimu ya sheria kupitia huduma za msaada wa kisheria (Legal Aid) pamoja na kuimarisha taasisi zinazohusika na utoaji wa haki na utawala bora.
“Hatuwezi kufikia maendeleo endelevu bila kuwepo kwa utawala wa sheria. Ndiyo maana Serikali inaendelea kuwekeza katika maboresho ya sheria na taasisi zinazohakikisha haki inapatikana kwa wananchi,” alisema Katimba.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mwanasheria wa Serikali ambao ndio waandaaji wa shughuli hiyo, Ado November amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mageuzi ya sheria na utekelezaji wa sera mbalimbali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, hatua ambazo zimechangia kuimarisha sekta za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ado alisema wamefanya kazi ya kuandika na kuhifadhi taarifa za mageuzi yaliyofanyika katika sekta mbalimbali, hususan afya, kwa kuonyesha utekelezaji wa sheria na maboresho yaliyofanyika tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani.
Alisema pamoja na kutekeleza sheria zilizokuwepo, Serikali imeendelea kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ili ziendane na mahitaji ya sasa pamoja na kuimarisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo na mipango mingine ya maendeleo.




