NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limesema litaendelea kuwa mdau muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia uwekezaji katika sekta za kilimo, ufugaji na uzalishaji wa mali.
Hata hivyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara maarufu sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam ya sabasaba JKT imefanikiwa kupata tuzo kwa kuwa mshindi katika sekta ya Kilimo.
Ushindi wao unatokana na juhudi kubwa katika kilimo biashara, ufugaji, uvuvi na uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa bora za viwandani ndani ya nchi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika maonesho hayo kuhusu mchango wa JKT katika kufanikisha dira hiyo, Mwenyekiti Kamati ya maonesho banda la JKT, Brigedia Jenerali Shija Lupi amesema taasisi hiyo imejijengea msingi imara katika uzalishaji wa kibiashara na wa chakula, huku ikiendelea kutoa mafunzo kwa wananchi ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Amesema Dira ya Taifa 2050 imeainisha fursa nyingi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji, maeneo ambayo JKT imekuwa mstari wa mbele kuyatekeleza kwa vitendo.
“JKT imekuwa kinara katika uzalishaji. Tunafanya kilimo kwa vitendo kupitia mashamba makubwa ya uzalishaji wa mali, tunazalisha mazao mbalimbali kwa ajili ya biashara na chakula, lakini pia tunatoa elimu na mafunzo kwa wananchi wanaotaka kufanya vizuri katika kilimo na ufugaji,” amesema.
Ameeleza kuwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakifika katika mabanda ya JKT kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa jeshi hilo, huku huduma hizo zikitolewa bila malipo.
Aidha, amesema kupitia kampuni ya SUMA JKT, taasisi hiyo imeendelea kushiriki katika kufunga mitambo ya kisasa pamoja na kujenga mabwawa ya ufugaji wa samaki, hatua ambayo imewanufaisha wananchi wengi kwa kuongeza ujuzi na uzalishaji.
Kwa mujibu Brigedia Jenerali Lupi amesema juhudi hizo zinaifanya taasisi hiyo kuwa miongoni mwa wadau muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050, hasa katika kuimarisha usalama wa chakula, kukuza biashara na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa nchi.

