NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamekuwa chachu ya maendeleo ya uchumi kwa kipindi cha miaka 50, yakisaidia kukuza uzalishaji, biashara, uwekezaji, ajira na kuunganisha Tanzania na masoko ya dunia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa ufunguzi wa Maonesho hayo, Rais Samia alisema maadhimisho hayo hayahusu historia ya maonesho pekee, bali ni ushuhuda wa mchango mkubwa wa sekta binafsi, wafanyabiashara, vijana na wajasiriamali katika kukuza uchumi wa taifa.
Alisema maonesho hayo yameendelea kuwa daraja muhimu linalounganisha wazalishaji na walaji, wafanyabiashara na masoko, pamoja na wawekezaji na fursa za biashara ndani na nje ya nchi.
“Tunapoadhimisha miaka 50 ya maonesho haya, tunalenga kulinda historia yake na kuthibitisha kuwa haibaki kwenye kumbukumbu pekee, bali inatafsiriwa katika kukuza uzalishaji, biashara, uwekezaji, ajira, usafirishaji na kuimarisha ustawi wa watu wetu,” alisema Rais Samia.
Alibainisha kuwa kupitia Sabasaba, wafanyabiashara wadogo wamekua na kuwa wafanyabiashara wakubwa, huku wakulima, wajasiriamali na wabunifu wakipata masoko mapya, mitaji na washirika wa biashara waliowawezesha kupanua shughuli zao.
Rais Samia pia alitumia nafasi hiyo kuelezea historia yake binafsi katika maonesho hayo, akisema aliwahi kushiriki kama afisa wa kawaida na baadaye kusimamia mabanda ya biashara, jambo linalodhihirisha nafasi muhimu ya Sabasaba katika kukuza vipaji na fursa za maendeleo.
“Nimefurahi kuona baadhi ya waonyeshaji ambao walikuwepo tangu nilipokuwa afisa wa kawaida bado wanaendelea kushiriki hadi leo, huku biashara zao zikiendelea kukua,” alisema.
Aidha, alisema maonesho ya mwaka huu yameendelea kuvutia washiriki wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania, jambo linaloonesha kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Alisema ushiriki mkubwa wa mataifa mbalimbali, ikiwemo Indonesia, unaonesha kuwa Tanzania inaendelea kuaminika kama kituo muhimu cha biashara, uwekezaji na lango la kufikia masoko ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la Afrika kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Rais Samia aliwapongeza viongozi na watumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, sekta binafsi, wadhamini, washirika na wadau wote waliowezesha kuanzishwa na kuendelea kuimarika kwa maonesho hayo kwa nusu karne.
Pia alitoa pongezi kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa maboresho yaliyofanyika katika miundombinu, matumizi ya teknolojia na uendeshaji wa maonesho hayo, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuyaendeleza ili yafikie viwango vikubwa zaidi vya kimataifa.
“Tuendelee kujitolea kwa nguvu zaidi ili kuyawezesha maonesho haya kufikia hatua kubwa zaidi na kuwa miongoni mwa maonesho yanayotambulika duniani,” alisema Rais Samia.
Kwa upande wake Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo amesema alimpongeza Rais Samia na Watanzania kwa kuadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya Maonesho ya Sabasaba, akisema mafanikio hayo yanaashiria miaka 50 ya dhamira ya Tanzania katika kukuza biashara, viwanda, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.
Alisema kuadhimisha miaka 50 ya Sabasaba si kusherehekea maonesho ya kimataifa pekee, bali ni kutambua taasisi iliyokua sambamba na mabadiliko ya uchumi wa Tanzania na ambayo sasa imejidhihirisha kuwa moja ya majukwaa muhimu zaidi Afrika katika kukuza biashara, ubunifu, viwanda na uwekezaji.
Chapo alisema kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu inayohusu mageuzi ya viwanda, ubunifu wa teknolojia, uunganishaji wa mifumo ya usafirishaji na kurahisisha biashara za mipakani inaakisi changamoto na vipaumbele ambavyo Afrika inapaswa kuvipa kipaumbele ili kujenga uchumi imara, shindani na unaounganishwa zaidi.
Alieleza kuwa Tanzania na Msumbiji zimeunganishwa kwanza na historia kabla ya kuwa washirika wa kiuchumi, akibainisha kuwa mataifa hayo yalikuwa washirika katika mapambano ya ukombozi wa taifa kabla hata ya kusaini mikataba ya ushirikiano.
“Kabla ya kuzungumzia njia za usafirishaji na minyororo ya thamani katika biashara, watu wetu tayari walikuwa wakitembea pamoja bega kwa bega wakitetea uhuru, ukombozi na heshima ya Waafrika chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na Eduardo Mondlane,” alisema Rais Chapo
Rais Chapo alisema Tanzania ina nafasi ya pekee katika mioyo ya wananchi wa Msumbiji kutokana na mchango wake katika harakati za ukombozi wa taifa hilo.
Alikumbusha kuwa Tanzania ndiyo iliyowapa hifadhi wapigania uhuru wa Msumbiji na kuwa makao ya Chama cha Ukombozi wa Msumbiji (FRELIMO), ambacho kilipata msaada wa kisiasa, kidiplomasia na kibinadamu uliowezesha taifa hilo kupata uhuru wake.
“Uhuru wa Msumbiji una alama za Tanzania. Wananchi wa Msumbiji hawatasahau kuwa wakati uhuru ulikuwa bado ndoto, Tanzania ilisaidia kuigeuza ndoto hiyo kuwa uhalisia,” alisema Chapo.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga alisema kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita TanTrade imekuwa daraja muhimu la kuitangaza Tanzania katika masoko ya dunia kupitia bidhaa, huduma na fursa mbalimbali za uwekezaji.
“Miaka 50 iliyopita TanTrade ilianzishwa kwa lengo la kuitangaza Tanzania, lakini miaka 50 ijayo tumejipanga kuhakikisha tunatafuta masoko kabla bidhaa hazijazalishwa. Dunia ya leo haiuzi bidhaa zilizozalishwa, huzalisha bidhaa zinazohitajika na soko,” alisema Kapinga.
Waziri huyo alisema maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa kielelezo cha safari ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa kuonyesha hatua iliyofikiwa na nchi pamoja na mwelekeo wa siku zijazo.
Alibainisha kuwa maonesho hayo yanaonesha wazi kuwa ustawi wa taifa hautegemei matumizi pekee, bali uwezo wa kuzalisha, kuongeza ushindani na kutumia fursa zilizopo katika masoko ya dunia.

