NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WATANZANIA wametakiwa kuwakataa wale wote wanaohamasisha au kuunga mkono mikakati inayolenga kuingiza nchi kwenye machafuko, vurugu au migawanyiko ya kisiasa.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea Bavicha Taifa, Masoud Mambo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema watu wanaofanya hao ni wapinga maslahi ya taifa na ustawi wa wananchi hivyo wanapaswa kukataliwa.
Amesema kuwa bila amani hakuna haki, bila utulivu hakuna maendeleo na kwamba bila umoja wa kitaifa hakuna Tanzania imara.
“Tanzania imekuwa kimbilio la watu waliokimbia machafuko ya kisiasa katika mataifa yao, tusikubali historia hii tukufu ibadilishwe kwa matakwa ya kisiasa ya muda mfupi.
“Watanzania tukumbuke tukiruhusu siasa za kuvuruga amani zitawale, waathirika wa kwanza tutakuwa ni sisi wenyewe sio hao walioughaibuni au wanasiasa wenye viza tayari kukimbilia ughaibuni. Maendeleo yatasimama, uchumi utadorora na ajira zitapotea hivyo gharama ya kuyajenga upya itabebwa na sisi wananchi,” amesema
Amesisitiza kuwa kwa miongo mingi Tanzania imejenga heshima kubwa kimataifa Kama nchi ya amani, umoja na utulivu wa kisiasa na kwamba sifa hiyo haikuja kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya umadhubuti wa Serikali, busara za viongozi na uzalendo wa wananchi.
Aidha amesema kuwa changamoto za kisiasa hazitatuliwi kwa maandamano na hamasa za uvunjifu wa amani, lugha za uchochezi au kampeni za kuichafua nchi ndani na nje ya mipaka bali zinatatuliwa kwa kutumia meza ya mazungumzo na majadiliano ya wazi kwa hoja na ustahimilivu.
“Tunaweza kutatua changamoto za kisiasa pia kwa mifumo ya kisheria iliyopo, elimu ya uraia kwa wananchi kupitia kampeni zenye kujenga hoja ili wapime na kuamua kwa busara,” amesema
Amefafanua kuwa Tanzania ni nchi inayotawaliwa na sheria, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, vyama vyote vilivyosajiliwa kisheria ni sawa mbele ya sheria bila ubaguzi wowote.
“Hivyo basi jaribio lolote la kubeza, kudharau au kupuuza ushiriki wa vyama fulani vya siasa katika chaguzi, mijadala au majukwaa ya kitaifa kwa hoja kwamba chama au vyama vingine vimesusa ni kinyume cha msingi ya demokrasia, haki na usawa,” amesema

