NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAKRISTO duniani kote huadhimisha Sikukuu ya Krismasi Desemba 25 kila mwaka, siku ambayo huwaleta pamoja kwa kula, kunywa na kubadilishana zawadi.
Katika kuelekea sherehe hizo, Kwaya ya Flying Family imeandaa tamasha maalum la muziki wa Classical litakalofanyika Desemba 7, mwaka huu, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Kwaya hiyo inajumuisha waimbaji kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ikiwa na lengo la kudumisha umoja na upendo miongoni mwa waumini kupitia muziki. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018, Flying Family imeandaa matamasha nane makubwa yaliyowakutanisha waumini, viongozi wa dini na serikali kwa pamoja.
Tamasha la Classical Music
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Innocent Fundisha, amesema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri, hivyo anawaomba watu kujitokeza kwa wingi kuja kumsifu Mungu kwa njia ya uimbaji.
Amesema licha ya ugumu wa kujifunza muziki wa Classical, wanakwaya wamethibitisha uwezo wao kwa kufanya mazoezi ya kiwango cha juu kwa lengo la kuwaburudisha wageni na kumsifu Mungu katika roho na kweli.
“Wanakwaya hawa wanajifunza nyimbo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii na kukutana kila Jumapili kwa mazoezi ya pamoja ya kuunganisha nyimbo hizo,” amesema Fundisha
Hata hivyo amesema tamasha la mwaka huu ni la kipekee kwani litahusisha nyimbo za watunzi maarufu wa muziki kama George Handel, Wolfgang Mozart, Johan Bach, Joseph Haydn, Felix Mendelssohn na Antonio Vivaldi, pamoja na kazi za watunzi wa Tanzania wakiwemo David Wasonga, John Mgandu, Egidius Mushumbusi na Mathias Msafiri.
Tiketi na Viingilio
Amesema tiketi za tamasha zinapatikana katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Kanisa Katoliki St. Peter Osterbay, KKKT Msasani, Paones Posta (Samora Tower), KKKT Goba, Kanisa Katoliki Mwenge na Kanisa la Anglican Ilala.
“Viingilio ni Sh. 50,000 kwa wakubwa, Sh. 30,000 kwa watoto, na Sh 100,000 kwa watu wa VIP, siku ya tamasha, kutakuwa na chakula na vinywaji vya kutosha kwa washiriki wote kama sehemu ya shamrashamra za msimu wa sikukuu,” amesema Fundisha
Viongozi Kutoka Madhehebu Mbalimbali Kuhudhuria
Hata hivyo Fundisha amesema tamasha hilo linatarajiwa kuhudhuria na viongozi mbalimbali wa dini akiwemo Askofu Thaddaeus Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Askofu Alex Malasusa wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, na Askofu Jackson Sosthenes wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Dar es Salaam.
“Pia maaskofu wasaidizi, mapadre, wachungaji, viongozi wa serikali, wanadiplomasia, wakuu wa mashirika, pamoja na waumini kutoka mikoa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki,” amesema
Lengo la Kwaya
Fundisha amesema Flying Family imeanzishwa kwa madhumuni ya kuleta umoja na mahusiano bora kati ya madhehebu ya Kikristo kupitia kushirikiana vipaji vya muziki.
“Kwaya yetu inawaleta pamoja wakristo wa madhehebu matatu, tunaungana na kumtangaza kisrto, lakini tuhahimiza umoja na undugu daima,” amesema na kuongeza
“Kwaya ina Bodi ya Wadhamini yenye wajumbe tisa wanaosimamia ustawi wa kwaya, ikiwa na jukumu la kupanga mikakati endelevu na kuweka dira ya maendeleo,” amesema
Mazoezi na Utendaji
Kwaya hufanya mazoezi kila Jumapili saa 9 alasiri hadi saa 12 jioni, ili kutoa nafasi kwa wanakwaya kuhudumu kwenye kwaya zao za Parokia na Makanisa wanapotoka. Sehemu kubwa ya mazoezi hufanyika kupitia WhatsApp, ambapo kila sauti ina kundi lake linalosimamiwa na mwalimu wake.
Fundisha amesema walimu wa kwaya wanatumia mbinu mbalimbali za kisasa ikiwa ni pamoja na kurekodi sauti, kutuma mifano ya nyimbo na kurekebisha makosa ya wanakwaya kwa njia ya mtandao.
Matarajio ya Kimataifa
Kwaya hiyo inalenga kutambulika kimataifa kupitia ubora wa muziki wake na matamasha ya kiwango cha juu. Fundisha amesema dhamira yao ni kuhakikisha Flying Family inakuwa alama ya ubora na umoja wa Kikristo kupitia muziki.
Wito kwa Wakristo na Vijana
Fundisha ametoa wito kwa vijana kutumia vipaji vyao kumtukuza Mungu kupitia muziki, akisema kufanya hivyo kunawasaidia kuepuka vitendo viovu na kujenga maadili mema.
Pia amewataka Wakristo kutambua kuwa wote ni kondoo wa Bwana Yesu Kristo hivyo wajenge ushirikiano bila kujali tofauti za kimadhehebu.
Aidha, anawakaribisha wenye vipaji vya uimbaji na upigaji vyombo kujiunga na kwaya hiyo kufuatana na taratibu zilizowekwa.
Shukrani na Uchangiaji
Kwaya imeishukuru jamii, viongozi wa dini na wadau mbalimbali kwa kuwaunga mkono katika shughuli zao, zikiwemo taasisi kama Paones General Trading.
Kwa wanaotaka kuchangia au kushiriki katika kuiwezesha kwaya hiyo, michango inaweza kutumwa kupitia: MPESA Lipa Namba: 5226676, NMB Akaunti: 22510097145 na Simu: 0764 088 006.





