NA FLORAH AMON,DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amehitimisha mgogoro wa nyumba kiwanja namba 819 Msasani Beach uliomhusisha mjane wa marehemu Justice Rugaobula, Alice Haule na Mohammed Mustafa Yusuf Ali ambapo amemkabidhi hati maalum iliyotolewa na wizara ya Ardhi ambayo inamtambilisha Alice Haule ndiye msimamizi halali wa mirathi kisheria baada timu ya wataalamu aliyoiunda kujiridhisha kuwa mjame huyo ndiye anaepaswa kukabidhiwa umiliki wa nyumba hiyo kama msimamizi wa mirathi.

Akizungumza leo Oktoba 20,2025 jijini Dar es Salaam RC Chalamila amesema baada ya kuibuka kwa mgogoro huo wa nyumba aliamua kuunda timu maalum ya wataalamu iliyohusisha wataalamu kutoka ofisi ya kamishna wa ardhi, jeshi la polisi na mawakili kutoka pande zote za mgogoro ambapo timu hiyo imejiridhisha kuwa Alice ndio mwenye haki kwenye nyumba hiyo kama msimamizi wa mirathi ya marehemu mumewe bwana Justice Rugaobula

Aidha RC Chalamila baada ya kumkabidhi hati miliki iliyoandikwa jina lake Alice kama msimamizi wa mirathi amemkabidhi pia mjane huyo kiasi cha Sh.Milioni 10 kama kifuta machozi kitokana na usumbufu alioupata na amemtaka Mohammed Mustafa Yusuf Ali kufika ofisini kwake ndani ya muda wa siku tano kwani muda wote wa kuendesha shauri hilo amekua akitafutwa na hajawahi kutokea lakini pia anatuhuma za kutumia vibaya majina ya viongozi.

Kwa upande wa Naibu Kamishna wa ardhi Mkoa wa Dar es salaam Shukrani Kyando akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya ardhi ameeleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa hadi kufikia maamuzi ya kumkabidhi nyumba hiyo Alice ambapo amesema nyumba hiyo haikuuzwa kisheria kwani fedha walizopeana ni za kukopeshana lakini pia hakuna sehemu Alice alishiriki uuzaji wa nyumba hiyo ya wanandoa

Mara baada ya maamuzi hayo kutolewa Alice kukabidhiwa hati miliki ya nyumba hiyo mjane huyo amemshukiru Rais Dk.Samia na Mkuu wa mkoa Dar es salaam kwa kumuwezesha kupata haki hiyo na amebainisha kuwa kwa sasa anaishi na watoto wanne wawili amezaa na marehemu mumewe lakini wawili ni watoto wa marehemu mumewe aliozaa na mwanamke mwingine


