
NA FLORAH AMON, DAR ES SALAAM

SERIKALI imeanza mkakati wa kushirikisha sekta binafsi katika kuandaa vijana wenye ujuzi, ubunifu na umahiri unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, hatua inayolenga kuondoa pengo la ajira kati ya wahitimu na waajiri.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mageuzi mapya katika mfumo wa elimu ya ufundi stadi ili kuhakikisha vijana wanapata mafunzo yanayoendana na mazingira halisi ya kazi.

“Mkutano huu ni jukwaa muhimu la kuunganisha elimu na viwanda tunataka kuona vijana wetu wakitoka vyuoni wakiwa tayari kufanya kazi, si kuanza kujifunza tena kazini,” amesema Prof. Nombo na kuongeza kuwa serikali imejizatiti kuboresha mitaala na kuongeza miundombinu ya vyuo ili kufanikisha mabadiliko hayo.
Prof. Nombo amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023) imeweka kipaumbele katika elimu yenye ujuzi na tija, huku serikali ikiendelea kuongeza idadi ya vyuo vya VETA na programu za mafunzo kwa vitendo ili kukidhi mahitaji ya ajira ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Clotilda Ndezi, amesema bodi inaendelea kusimamia utekelezaji wa mafunzo ya vitendo kwa kushirikisha viwanda, waajiri na taasisi za mafunzo, ili wahitimu wawe na ujuzi halisi unaohitajika kazini.
“Tunataka kuondoa pengo kati ya darasani na kiwandani pia wakufunzi wa VETA kupewa fursa ya kujifunza teknolojia mpya katika maeneo ya kazi, ili watoe mafunzo yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.Amesisitiza Ndezi
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema katika kipindi cha miaka mitano, idadi ya vyuo vya VETA imeongezeka kutoka 37 hadi 80, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa wadau wa viwanda na sekta ya elimu ni nyenzo muhimu katika kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea ujuzi.
Akihitimisha, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Serera, amesema ukuaji wa sekta ya viwanda unategemea nguvu kazi yenye ujuzi wa vitendo, hivyo serikali itaendelea kuimarisha elimu ya ufundi stadi kama chachu ya ajira, ubunifu na maendeleo ya uchumi wa nchi.

