NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM

SERIKALI kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga jumla ya Sh. Bilioni 18 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo ya bajaji na pikipiki kwa vikundi sita Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema fedha hizo zimetengwa kama sehemu ya bajeti ya Wilaya kwa mwaka huu wa fedha, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha wananchi kupitia mikopo isiyo na riba.

“Kwa sasa tupo katika awamu ya kwanza ya mpango huu. Tumepokea zaidi ya maombi 120 yenye thamani ya takribani Sh.Bilioni 3. Wanavikundi
watakaonufaika watakabidhiwa pikipiki 39 na bajaji 6 zenye thamani ya zaidi ya milioni 240,” amesema Mpogolo.

Mpogolo ameeleza kuwa mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na CRDB Bank Foundation, ambayo imepewa jukumu la kusimamia utoaji na urejeshaji wa mikopo hiyo ameongeza kuwa wanufaika wote wamepatiwa mafunzo ya biashara, elimu ya fedha, na kufunguliwa akaunti maalum kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu na kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa, amesema taasisi hiyo imejipanga kikamilifu kusimamia mpango huo kwa uwazi, ufanisi na kwa kushirikiana kwa karibu na halmashauri.
“Hatujatoa mikopo tu. Tumewekeza pia katika elimu ya fedha, kutembelea vikundi, na kuanzisha mifumo madhubuti ya ufuatiliaji ili kuhakikisha kila mkopo unaleta matokeo chanya kwa wanufaika na jamii kwa ujumla,” amesema Mwambapa.

Nao Wanufaika wa mikopo hiyo walitoa shukrani kwa Serikali na CRDB Foundation kwa fursa hiyo, huku wakiahidi kufanya marejesho kwa wakati ili kuwezesha vikundi vingine kufaidika na mpango huo pia wamesisitiza kuzingatia sheria za usalama barabarani katika matumizi ya vyombo vya moto walivyokabidhiwa.

Mpango huu wa mikopo ya asilimia 10 ni miongoni mwa mikakati ya kitaifa ya kuwawezesha Watanzania kiuchumi, hasa makundi maalum, kwa kuwapatia mitaji na nyenzo muhimu za kuanzisha au kukuza shughuli zao za ujasiriamali.


