NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imetoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika masuala ya Nishati Safi kutokana na kuwepo mikakati imara, mazingira wezeshi, amani na utulivu inayotoa fursa kwa maendeleo ya kiuchumi.
Pia ameweka wazi kwamba kutokana na kuwepo kwa mazingira wezeshi, amani na utulivu shughuli za uzalishaji katika mkondo wa Juu wa Petrol kwenye nyanja ya ajira imeongezeka kutoka asilimia 55 hadi 85.
Mhandisi Charles Sangweni amebainisha hayo leo, Julai 9, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutembelea mabanda yaliyopo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.
“Tangu mwaka 2017 tumekuwa tukishiriki maonesho haya na mwaka huu yamekuwa wa mazuri kutokana na kuendeshwa kidigitali zaidi na tutaendelea kushiriki kwa mafanikio makubwa na kwa mwaka huu tumepata maswali mazito kutoka kwa wananchi wanaofika kutembelea banda letu kuhusu nishati safi na tumewajibu kwa mapana na ninaamini wameridhika,” amesema.
Aidha alijinasibu kuwa wakati Mamlaka hiyo wakati inaanzishwa ilikuwa na watumishi 45 na sasa wamefikia 95 jambo ambalo kwao ni mafanikio makubwa na wanamshukuru Rais samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji ambao ameufanya katika mamlaka hiyo.
“Tunamshukuru Mhe Rais, kwani amefanya kazi kubwa katika uwekezaji katika mamlaka hii kwani kuanzia mishahara na uwepo wa mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji, hivyo ni wakati wao wawekezaji kuitumia nafasi hiyo kuja kuwekeza hapa nchini hususan katika Nishati Safi,” amesema.
Pia ameongeza kuwa kwa kati ya kampuni 10 zinazoshughulika na utafutaji mafuta na gesi sita ni za kitanzania na hiyo inatokana na kuwepo mpango wa mkakati wa kuhakikisha vyuo vya Tanzania zifundisha kozi za mafuta na gesi na wahitimu wanapomaliza masomo yanaingia moja kwa moja kufanya shughuli hizo.
Mha. Sangweni kwa sasa wapo katika mchakato wa kuchimba visima vitatu vya gesi asilia mkoani Mtwara unaotarajia kuanza Novemba mwaka huu unaotarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kutoka kitalu cha Mnazi Bay kwa zaidi ya ujazo wa milioni 30 kwa siku jambo ambalo litakuwa ni mafanikio ya kujivunia.