NA ANDREA NGOBOLE,BABATI,MANYARA
CHEM CHEM Safari lodge iliyopo wilaya ya Babati mkoa wa Manyara, imeeleza siri ya kushinda tuzo mbili za kimataifa ya lodge bora ya kifahari Tanzania na Lodge bora ya kifahari Afrika, (luxury safari lodge Award) ambayo imetolewa kwenye Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) zilizofanyika jijini Dar es Saalam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Tuzo hizi zimefanyika kwa mara ya kwanza nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 na kushirikisha hifadhi za Taifa, sekta za Utalii Duniani na Wawekezaji katika sekta hiyo.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari Mkuu wa wilaya ya Babati Emmanuela Mtatifikolo na Meneja wa Huduma wa hotel hiyo, Jorg Weytjens walisema siri kubwa ya ushindi huo wa tuzo mbili kwa Pamoja tuzo ya hoteli bora ya kifahari Tanzania na Lodge bora ya Kifahari Afrika, unatokana na huduma bora Upendo,nidhamu, kujituma na ushirikiano.
Mtatifikolo alisema Chemchem Safari Lodge ambayo ipo kati kati ya hifadhi za Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Manyara, katika eneo la Jumuiya ya hifadhi ya jamii ya Wanyamapori Burunge,(Burunge WMA) imetunzwa katika mazingira ya asili kabisa na ukiwa ndani ya hoteli unashuhudia makundi ya wanyamapori kwa karibu zaidi.
“Licha ya kuwa na huduma nzuri na bora kabisa Afrika na uwekezaji bora uliofanywa na wamiliki wa hoteli hiyo, Fabia Bausch na Nicolaus Negre kuvutia maelfu ya wageni lakini serikali ya Rais Samia Suluhu imeweka mazingira mazuri sana kuwezesha watalii kuja Tanzania na kuitangaza vizuri Tanzania”alisema
Alisema kwa wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara, chini ya uongozi wa Mkuu wa mkoa Queen Sendiga umeendelea kuwekwa mazingira bora ya kuendeleza Uhifadhi na Utalii ili kuvutia watalii kutembelea mkoa huo na sasa mafanikio yameanza kuonekana.
Alisema licha ya uwekezaji wa hoteli Chem chem wamekuwa wakifanya Utalii wa picha katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya wanyamapori, ziwa na vivutio kadhaa vya watalii, eneo ambalo serikali imeendelea kulitunza ikiwepo kudhibiti matukio ya ujangili, uharibifu wa mazingira na kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi.
Kwa upande wake, Weytjens alisema siri nyingine ya ushindi ni huduma bora na ukarimu ambao wanapata wageni mashuhuri duniani wanaotembelea hoteli hiyo yenye hadhi ya kimataifa.
“Tunatoa huduma bora kabisa,wafanyakazi wanajituma sana kuwakarimu wageni lakini pia kuna ushirikiano mkubwa baina yetu kama hoteli, jamii inayozunguka hoteli,serikali ya Rais Samia Suluhu na wadau wengine”alisema
Meneja wa Chem Chem lodge, Elizabeth Wambui wamefurahi sana kupata tuzo hiyo kubwa mwaka huu, ambayo ni kati ya tuzo bora Afrika ambazo wamekuwa wakipata katika miaka ya karibuni.
“Tumefurahi kupata tuzo hizi, hii ilikuwa ni ndogo ya waanzishi wa Chemchem Fabia na Nicolaus kutoa huduma bora kabisa Afrika na ndoto zao zimekuwa kweli”alisema
Wambui alisema wafanyakazi wa hoteli, Serikali na jamii nzima ya Burunge wamekuwa na ushirikiano mkubwa ambao umekuwa ukichangia hoteli hiyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wageni.
Mpishi Mkuu wa hoteli hiyo, Jimmy Ngira alisema chakula bora ambacho wamekuwa wakiandaa kimekuwa pia kivutio kikubwa cha watalii na wageni wengine duniani.
“Tulishinda pia mwaka jana hoteli ambayo inatoa chakula bora Afrika na ushindi huu wa sasa ni sehemu ya mafanikio kwani unatokana na maoni ya watalii wanaotembelea hoteli hiyo”alisema
Ngira alisema wafanyakazi wa idara zote za Chemchem lodge wamekuwa wakifanyakazi kwa upendo, kujituma na wamekuwa na nidhamu kubwa ambayo imekuwa ikiwavutia watalii na wageni kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Katika tuzo hizo mwaka huu Tanzania iliweka rekodi mpya kwa kushinda jumla ya tuzo 27 duniani, serikali ikinyakuwa tuzo 11 zikiwepo na vivutio bora vya Utalii,bodi bora ya Utalii, Nchi bora ya Utalii Afrika wa safari Pamoja na viwanja vya ndege bora vikiwepo ya hifadhi za Taifa.
Sekta binafsi katika tuzo hizo, ilitwaa tuzo 16 zikiwepo za hoteli bora, kampuni bora za Utalii wa Safari,hoteli zenye huduma bora,hoteli zenye fukwe bora zinazovutia maelfu ya watalii duniani.