NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan
amemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara,Dk. Selemani Jafo kuliangalia vema suala ya wageni waliopo Kariakoo kufanya biashara zinazofanywa na wenyeji.
Rais Samia ametoa kauli hiyo mara baada ya kupokea kero hiyo kutoka kwa Mwenyeki wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi ambaye alimuomba rais kuwasaidia katika jambo hilo.
Akizungumza leo Januari 30, 2025 wakati akishiriki chakula cha mchana na waokoaji wa Kariakoo, Rais Samia amesema kuna kipindi alirushiwa video fupi ambayo ilimuonesha mgeni akipigana na mwenyeji kariakoo na alipouliza kwanini wanafanya hivyo alijibiwa kuwa huyo ni mmachinga na wameshindwana katika biashara yao.
“Sasa haiwezekani mgeni akawe mmachinga, tukiruhusu hilo vijana wetu hapa nchini watafanya kazi gani kwahiyo Waziri simamia hilo jambo,” amesema Rais Samia
Rais Samia amesema katika Jiji la Dar es Salaam kuna Mradi wa Kuendeleza Miundombinu ( DMDP) ambao kati ya fedha za mradi huo Serikali imejipanga kujenga soko jingine kubwa kama la Kariakoo eneo la Jangwani.
Amesema ni maoni yao kwamba baadhi ya wafanyabiashara wakiwemo wamachinga tutawahamisha na kupelekwa jangwani ili wakafanye biashara zao kwa nafasi bila buguza.
Hata hivyo Rais Samia amesema kuwa wafanyabiashara ndogondogo na wa kati wanakimbia kulipa kodi na kwamba kama hawatalipa kodi hizo na kuwaacha wachache kulipa itakuwa hasara kubwa kwa Taifa.
“Wajibika kwa serikali yako ili mambo yawe mazuri, kwa kulipa kodi tutalinda nchi yetu kuwa omba omba na kupunguza mikopo maana tunakopa kujenga na kuitengeneza nchi, wengine wasiojua wanasimama kusema hii serikali kazi kukopa kwani tunakopa kununua sare za harusi.
“Tunakopa kujenga reli, barabara, shule, vituo vya huduma za afya, tunakopa kufanya mji wa Dar s Salaam na Dodoma kuwa miji inayoheshimika na kukuza hadhi ya nchi yetu, mtusaidie kila anayefanyabiashara akichangia kidogo kiwango cha kukopa kitapungua na tutaendesha mambo mengi kwa fedha tunazokusanya ndani,” amesema Rais Samia
Rais Samia amesema hakuna anayependa kukopa bali wanafanya hivyo kwa sababu na kusisitiza kuwa wanazungumzia kukua kwa ukusanyaji wa kodi kwani kwa sasa hivi TRA inakusanya Trilioni 3/-kwa mwezi huku lengo likiwa kufikia Trilioni 4/- kwa mwezi kwa miaka ijayo.
Aidha amesema tukio la Kariakoo limewakumbusha na kuwapa somo kubwa kuhusu umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa na kuhakikisha wanakuwa na utayari wa kukabiliana na dharura wakati wowote.
“Tumepata somo jinsi biashara inayoendeshwa pale Kariakoo, tumeelezwa hapa lile jengo lilikuwa na uwezo wa kuchukua tani 250 za mizigo lakini tani zilizokuwepo pale ni 800, kwahiyo kwa namna yoyote ile lisingeweza kubeba, sasa hilo ni jengo moja nina hakika majengo mengi yapo katika mfumo huo,” amesema Rais Samia
Amesema jambo jingine ambalo wamepata somo ni usimamizi wa serikali wakati wa ujenzi na kuhakikisha viwango vya ujenzi vinafuatwa.
“Kwa wale walioliona jengo unaona kabisa ni mchanga mwingi kuliko nondo na saruji. Somo jingine nililoliona ni mali inayofichwa mule ndani bila kulipiwa kodi, sidhani zile tani 800 zilizokuwepo zimelipwa kodi na huo ndio ugomvi wa TRA na wafanyabiashara
Amesema jambo linapotokea kuna la kujifunza na mpango wa serikali baadaye ni kuhakikisha uwepo wa vifaa, rasilimali na utaalamu unaohitajika ili kukabiliana na maafa kwa ufanisi zaidi.
“Tunawashukuru sekta binafsi kwa kujitoa kwa hali na mali, ila vile vitu vingi vyao ilitakiwa Serikali tuwenavyo ila tunashukuru kitengo cha maafa ya uokozi, tumesoma somo letu na tulitakiwa sisi serikali tuwe navyo,” amesema