NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema mfumo wa kidijitali utakaomfanya mtumiaji wa huduma za kifedha kuwasilisha malalamiko utamuwezesha hata asiye na simu janja kutumia mfumo huo kutoa malalamiko yake.
Sambamba na hilo mfumo huo utazinduliwa katikati ya Mwezi Januari mwaka 2025.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Ustawi wa Huduma Jumuishi za Kifedha wa BoT, Nangi Massawe jijini Dar es Salaam leo Desemba 10, 2024, wakati akifungua Warsha ya siku mbili kuhusu mfumo wa malalamiko kwa Wawakilishi wa Taasisi za fedha.
Amesema mfumo huo uliotengenezwa na kukamilika ni muhimu sana kwa watumiaji wa huduma za kifedha ambapo pia hautawaacha nyuma hata wale walio vijijini.
” Hivi tunavyozungumza watu wapo kazini kuhakikisha hata yule mwenye kitochi anaweza kutumia mfumo huu hivyo ni matarajio yangu kwamba kupitia warsha hii wote tunapata ueelewa mzuri na kuanza kuutumia kabla ya kuuzindua.”amesisitiza
Kwa upande wake Kaimu Meneja Idara ya Ulinzi wa Watumiaji wa Fedha, (Financial Consumer Protection), Dk Hadija Kishimba, amesema BoT imeandaa warsha hiyo kwa taasisi za fedha ili kuuelewa mfumo kwani wao ndio wanaokutana na wateja.
“Tunapaswa kuuelewa mfumo kwa sababu tunakwenda kusogeza huduma kwa walaji tunataka mwananchi alalamike kupitia kiganja chake.
“Ninyi ndio wenye mfumo, nasema hivyo kwasababu ninyi ndio mnaokutana na wananchi, BoT imeandaa mfumo na tunapopeleka automation kwenye taasisi za fedha sio lengo la BoT kubaki na mfumo huo, lengo letu wananchi watumie ili na sisi tupate mrejesho.” amesema.
Naye mtoa Mada juu ya Mfumo huo ambao utazinduliwa rasmi Januari mwakani Laura Mandari amesisitiza kuwa mfumo huo umeshakamilika takribani miezi miwili iliyopita na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni kujenga uelewa kwa Taasisi za Fedha na wananchi kwa ujumla.