NA ANDREA NGOBOLE,ARUSHA
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Fredrick Shoo amewataka Vijana nchini, bila kujali dini zao, kujitambua na kujitokeza kugombea, kushiriki katika chaguzi ili wapate fursa ya kushiriki katika vyombo vya maamuzi.
Akifungua Warsha ya kitaifa ya vijana wa dini mbali mbali kutoka mikoa ya Tanzania bara na Visiwani, kuhusu masuala ya uongozi na ujenzi wa amani katika jamii ambayo iliandaliwa na kamati ya amani ya dini mbali mbali nchini iliyofanyika Corridor Springs Hotel Jijini Arusha.
Askofu Shoo alisema, vijana wanajukumu kubwa la kushiriki katika masuala ya ujenzi wa taifa badala ya kubaki wasikilizaji na kundi la walalamikaji.
“Vijana mnapaswa kujitambua na kuwa waadilifu na wazalendo katika taifa lenu lakini pia mnapaswa kushiriki katika uongozi na kutatua kero mbali mbali katika jamii”alisema
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Baraza la Waislamu nchini (BAKWATA) Sheikh Hamis Mataka alisema vijana wanapaswa kuzingatia maadili yao na kushiriki kulinda amani ya nchi.
Alisema hivi sasa Taifa linapita katika kipindi kigumu cha vijana wengi kuwa na tatizo la maadili jambo ambalo lazima libadilike kwani sehemu kubwa ya watu katika taifa hili ni vijana.
“Taifa linapaswa kuwa na vijana waadilifu, wanaojitambua na kushiriki vizuri katika masuala mbali mbali ya kuwaletea maendeleo”alisema
Kwa upande wake, Askofu mkuu wa kanisa la Mennonite Tanzania na Mwenyekiti wa kamati ya amani ya dini mbalimbali kuhusu haki za kiuchumi na maadili ya uumbaji, Nelson Kisare alisema ni wajibu wa vijana kutambua nafasi yao katika jamii.
“Tuwawakutanisha hapa vijana ili watambuwe nafasi yao katika jamii, vijana wawe waadilifu lakini kikubwa washiriki katika masuala ya kijamii ikiwepo masuala ya uongozi, kukabiliana na changamoto kadhaa ikiwepo mabadiliko ya tabia nchi” alisema
Askofu Kisare alisema vijana wanaojitambua ndio wanaweza kuleta mabadiliko katika taifa lolote, kuleta amani na maendeleo katika taifa”alisema
Mmoja wa vijana wanaoshiriki Warsha hiyo,Yusuph Mbaruku kutoka Pemba alisema anaishukuru kamati ya Amani ya dini zote kuwakutanisha vijana na kuwapa elimu juu ya kujitambua na kuwa waadilifu na wazalendo katika Taifa la Tanzania.