NA ANDREA NGOBOLE,ARUSHA
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan amewataka Madaktari wa mifugo nchini kushiriki kampeni kabambe ya utoaji chanjo ya magonjwa ya mifugo ili kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya kipaumbele kwa mifugo nchini na kuongeza tija ya uzalishaji wa mifugo na kuongeza kiwango cha uuzaji wa mazao yake ndani na nje ya nchi.
Aidha amefurahishwa na kaulimbiu ya kongamano la kisayansi la 42 la chama cha madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) inayosema ‘’TOKOMEZA MAGONJWA YA MIFUGO ILI KUONGEZA TIJA YA UZALISHAJI NA KUIMARISHA BIASHARA YA MIFUGO NA MAZAO YAKE NDANI NA NJE YA NCHI” kwani inaendana na azma ya serikali ya awamu ya sita yenye lengo la kuboresha Maisha ya Mtanzania kwa kuimarisha sekta ya mifugo nchini baada ya kutenga fedha jumla ya billion 460 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwenye sekta ya mifugo na kati ya hizo bilioni 28.1 zitatumika katika kampeni ya kupiga chanjo mifugo kitaifa ili kutokomeza magonjwa ya kipaumbele ambayo ni kikwazo cha biashara ya mifugo nchini pia kutokomeza magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa Wanyama Kwenda kwa binadamu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa mifugo nchini Abdallah Ulega wakati akisoma hotuba ya mheshimiwa Rais Samia, wakati wa ufunguzi wa kongamano la siku tatu la kisayansi la 42 la chama cha madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) katika ukumbi wa hotel ya Ngurdoto iliyopo nje kidogo ya jiji la Arusha.
Waziri Ulega amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kutoa ajira za muda mfupi kwa vijana 3540 wataalamu wa Afya ya mifugo waliopo nje ya ajira rasmi katika mikoa yote Tanzania, pia zaidi ya Ng’ombe milioni 19 watachanjwa dhidi ya magonjwa ya mapafu, Mbuzi na Kondoo zaidi ya Milioni 20 watachanjwa chanjo ya ugonjwa wa sotoka na Jumla ya Kuku wa asili milioni 40 watachanjwa chanjo ya ugonjwa wa kideri.
Amewahimiza Madaktari hao zaidi ya 2000 walishiriki kongamano hilo kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika uzinduzi wa kampeni hiyo itakayozinduliwa mapema mwaka 2025 na kudumu kwa miaka mitano.
Awali akisoma risala ya kongamano hilo mwenyekiti wa chama hicho Professa Esron Karimuribo aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa juhudi kubwa ya kuboresha sekta ya mifugo kwa kutenga bajeti ya mifugo bilioni 460 ambayo ni ongezeko la asilimia 960 kutoka bajeti 2022/ 23 ambayo ilikuwa ni bilioni 47, Aidha aliipongeza kutengwa kwa bilioni 28 za mpango wa chanjo kabambe ya kutokomeza magonjwa ya kipaumbele kwa mifugo ambayo ni homa ya mapafu kwa Ng’ombe, Sotoka ya mbuzi na kondoo, Pamoja na chanjo ya kideri kwa Kuku wa asili ambapo madaktari hao wameahidi kushirikiana na serikali kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa kwa kadiri ya malengo ya serikali.
Aidha Profesa Karimuribo alisema bado kuna changamoto ya madakatari wa Wanyama katika maeneo hatarishi kutoka nje ya nchi hususani kwa mikoa ya mipakani kama Kagera, Mara, shinyanga, simiyu, Kigoma, Njombe, Rvuma na Iringa ambao hawana madaktari wa mikoa wenye jukumu la kushauri mamlaka ya mikoa namna bora ya kudhibiti magonjwa ya mifugo toka nchi Jirani na kuiweka salama mifugo ndani ya mikoa husika.
Waziri Ulega akijibu changamoto hiyo Madaktari wa Mikoa alimuagiaza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo Profesa Mdoe awasiliane na Tume ya ajira na Utumishi ili kupata kibali cha kuwapandisha Daraja Madaktari wa wilaya wanaofanya vizuri kuwa Madaktari wa mikoa husika na kuziba ombwe hilo.