NA MWANDISHI WETU,RUKWA
SERIKALI imesema kuwa mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa TAZA
unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti
400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga na kuunganisha Tanzania na Zambia
(TAZA) pamoja na vituo vya kupoza umeme vya Tagamenda, Kisada, Iganjo,
Nkengamo na Malangali utawezesha kuunganisha Bara la Afrika kwa
nishati ya umeme kutoka Afrika Kusini hadi Ethiopia.
Hayo yameelezwa leo Julai 29, 2024 Sumbawanga mkoani Rukwa na
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko wakati
akiweka jiwe la msingi la utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa
usafirishaji umeme ambao unahusisha kipande cha Kilometa 4 kutoka Tunduma hadi Nakonde mpakani mwa
Tanzania na Zambia.
“ Kwa kutambua kuwa nishati ni kichocheo cha uchumi, Serikali
imeendelea kutekekeza miradi mbalimbali ukiwemo wa Julius Nyerere
(JNHPP) ambao tayari unaingiza megawati 705 kwenye gridi ya Taifa na
hivyo kuwezesha nchi kuwa na ziada ya umeme huku mtambo mwingine wa
megawati 235 ukitarajiwa kuwashwa mwezi Agosti”, amesema Dk. Biteko.
Ametaja miradi mingine inayotekelezwa kuwa ni wa umeme Jua wa Kishapu
(MW 150), Malagarasi (MW 49.5) na ya Gesi Asilia huku lengo likiwa ni
kuwa na uhakika wa umeme wa kutosha.
Pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo, Dkt. Biteko amesema uzalishaji
wa umeme lazima uende pamoja na kazi ya uungashiaji umeme wananchi
kupitia miradi mbalimbali kama wa TAZA ambao unawahakikishia Wanarukwa
upatikanaji wa umeme wa gridi ambao utakuwa wa uhakika na wa kutosha.
Amesema kwa sasa Mkoa wa Rukwa unapata umeme kwa kiasi kikubwa kutoka
nchini Zambia kwa gharama ya Sh.Bilioni 15 kwa mwaka hivyo
kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Tanzania kuacha kununua umeme
kutoka nchi hiyo isipokuwa nyakati za dharura.
Ameongeza kuwa, mradi wa TAZA utafaidisha pia maeneo yanayopitiwa na
mkuza kutoka mkoani Iringa hadi Rukwa kupitia vituo vya kupoza na
kusambaza umeme na kuwezesha kufanyika kwa biashara ya umeme katika
nchi zilizopo Mashariki mwa Afrika kupitia Southern African Power
Pool (SAPP) na Easten Africa Power Pool (EAPP).
Kuhusu usimamizi wa mradi huo, Dkt, Biteko pamoja na kuipongeza
TANESCO kwa utendaji mzuri wa kazi, ameiagiza taasisi hiyo kuhakikisha
kuwa kasi ya utekelezaji mradi wa TAZA inaendelea kuwa kubwa, na
kwamba tukio la kuwekwa kwa jiwe la msingi lisiishie kwenye kupiga
picha na kisha kutokomea bali wausimamie mradi huo ili ulete matokeo
tarajiwa.
Akigusia usambazaji wa umeme vijijini mkoani Rukwa, Dk.Biteko amesema
kuwa Serikali haifurahishwi na kasi yake ya utekelezaji wa miradi
kwani analalamikiwa kusuasua na hivyo ameagiza kuwa ifikapo Agosti
mwaka huu awe amemaliza kazi na asipotekeleza agizo hilo achukuliwe
hatua za kimkataba na hii inajumusha pia wakandarasi wengine wazembe
ikiwemo katika Mkoa wa Kagera.
“Kazi za umeme vijijini zinaombwa na kampuni za nje ya nchi na
kampuni za ndani, tunaonekana wabaya kwa kuzibana sana kampuni za nje
lakini za ndani tunabembelezana, Katibu Mkuu na DG REA nataka nione
hatua zinachukuliwa, haiwezekani wakandarasi wageni tunawabana halafu
wa ndani wanaharibu miradit, wananchi wanalalamika halafu
tunabembelezana, hii hapana.” Amesisitiza Dk. Biteko
Amesema Serikali inataka kumaliza kazi ya usambazaji umeme vijijini na
kuhamia vitongojini na kwamba lengo ni kuwa ifikapo mwezi wa 12 mwaka
huu vijiji vyote viwe vimesambaziwa umeme.
Kuhusu utekelezaji wa TAZA, Dkt. Biteko ameshukuru Wafadhili wa mradi
huo ambao ni Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Ufaransa
(AFD), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) ambao kwa pamoja wametoa zaidi ya
shilingi Trilioni Moja za kutekeleza mradi huo ambao pia unahusisha
ujenzi wa vituo vitano vya kupiza umeme. Amesema Serikali ya Awamu ya
Sita inawajali Wafadhili wetu.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali
itaendelea kuipa kipaumbele ajenda husika kwani imeshaanzisha Kitengo
cha kushughulikia nishati hiyo ndani ya Wizara na kwamba Benki ya
Dunia imeahidi kuangalia namna ya kuiwezesha Serikali kutekeleza
ajenda hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere amesema mradi wa TAZA
utaihakikishia Rukwa umeme wa uhakika, pia kuimarisha uwekezaji ambapo
amemshukuru Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji
wa miradi ya umeme vijijini ambapo tayari vijiji 308 vina umeme huku
31 vilivyobaki kazi ikiendelea.
Kwa upande wake, Katibu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi
Mramba amesema mradi wa TAZA ni wa kipekee kwa sababu utawezesha
Afrika kuunganishwa na umeme kutoka Afrika Kusini hadi Ethiopia.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathew
Mkingule ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa
utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa umeme wa TAZA ambao
amesema utahakikisha usalama wa nishati katika nchi za Kusini mwa
Afrika, kukuza uchumi Mkoa wa Rukwa, kuwezesha biashara ya umeme,
fursa ya ajira na kulinda mazingira kwani nishati ya umeme inawezesha
wananchi kutumia nishati hiyo katika kupikia.
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete kwa niaba ya
Wawekezaji wa mradi amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Dk. Biteko pamoja na Serikali kwa ujumla kwa miongozo
ambayo imewezesha mradi wa TAZA kuanza kutekelezwa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga
alieleza kuwa, mradi wa TAZA ni sehemu ya maazimio ya yaliyofanyika
Desemba 15, 2014 baina ya Tanzania, Kenya na Zambia ya
kuunganisha gridi za nchi hizo tatu.
Katika utekelezaji wa makubaliano hayo, amesema Tanzania ilianza
kujenga laini ya umeme ya kV 400 ya km 670 kutoka Dodoma hadi
Shinyanga ambayo ilishakamilika na baadaye kujenga laini ya kV 400
kutoka Singida hadi Namanga kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya ambao
umekamilika kwa asilimia 99.8 na kipande cha tatu ni cha mradi wa
TAZA ambacho kinatekelezwa sasa ili kuunganisha gridi ya Tanzania na
Zambia.
Amesema mradi umeshaanza na umefikia asilimia 29.8 huku ukitarajiwa
kukamilika Mei 2026.
Wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Katibu MKuu
Wizara ya Nishati, Dktl. James Mataragio, Wenyeviti na Makamu Wenyeviti
wa kamati mbalimbali za Bunge ikiwemo ya Bajeti, Hesabu za Serikali,
Nishati na Madini, Mwakilishi wa AU, na AFD, Katibu Mtendaji wa EAPP,
Bodi na Wakurugenzi wa Taasisi chini ya Wizara, Menejimenti Wizara ya
Nishati pamoja na Watendaji kutoka Shirika la Umeme la Zambia (ZESCO).