NA MAGENDELA HAMISI,DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Kanisa la Jubilee linaloendesha shughuli zake za ibada katika Mtaa wa Pakacha Tandale Uwanja wa Fisi jijini Dar es Salaam umetakiwa kujipanga na kuunda vikundi ili kuchukua mikopo inayotolewa na Halmashauri ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Hayo yamebainishwa leo Julai 27, 20224 na Diwani wa Kata ya Hananasi, Kinondoni , Wlfred Nyamwija, aliyekuwa mgeni rasmi, akimwakilisha Diwani wa Kata ya Tandale katika shughuli ya kutoa misaada kwa makundi maalumu wanaoishi katika mtaa huo wakiwemo wazee, wajane, wanaoishi katika mazingira magumu na watoto.
“Nimesikiliza risala yenu na licha ya kufanya vema katika utoaji huduma za kiimani kwa wananchi hususani wanaoishi katika mazingira magumu na wale waliotumbukia katika tabia hatarishi bado mnakabiliwa na changamoto ya fedha za kuendesha shughuli zenu.
“Pia mnahitaji eneo kwa ajili ya kufungua kituo cha kulelea jamii inayoishi kwenye mazingira magumu, kufungua shule, sehemu ya kufungua viwanda vidogovidogo na shamba kwa ajili ya kilimo itakayosaidia kuwakamua kiuchumi na kuwaondoa katika dimbwi la umasikini.
“Haya yote yatafanikiwa ikiwa mtajipanga na kuchukua mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10 ambayo ipo mbioni kuanza kutolewa kwa mara nyingine baada ya kusimamishwa kwa muda, hivyo andikeni miradi nasi kwakuwa tunaingia kwenye vikao tutapiga chapuo ili mfanikiwe kupata na kuondoa changamoto zinazowakabili,” amesema.
Pia Diwani huyo, alitoa mchango wa Sh. 1,000,000 kwa kanisa hilo ili kusaidia kutatua changamoto ndogondogo huku kubwa zikiendelea kufanyiwa kazi ili kupambana kubadilisha fikra za baadhi wananchi wanaishi katika eneo hilo la Uwanja Fisi ambao kwa sasa umebadilishwa jina kuitwa Uwanja wa Sifa.
Kanisa hilo pia limesaidia nguo na viatu wazee, wajane, vijana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Msoma risala, Mchungaji Mary Mudirikati, amesema changamoto ya kukosa usafiri wao wenyewe, fedha za kuzunguka mikoani kwa ajili ya kutoa huduma imekuwa ikiwapa ugumu katika kutimiza malengo yao.
Pia ametoa wito kwa Serikali kuwasaidia vijana wanahudumiwa na kanisa hilo kuwapatia mafunzo ya ufundi na mitaji ili kuwasaidia kuwaondoa katika changamoto za utegemezi na kwenye dimbwi la umasikini na tabia hatarishi.
“Tunaishukuru Serikali kupitia Rais wetu mpendwa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada madhubuti kwa ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayosaidia kuinua uchumi wa nchi na kuwajengea mazingira rafiki vijana kushiriki katika ujenzi wa taifa.
“Ombi letu kwa Serikali ni kwamba tunaomba vijana hawa waonewe huruma na viongozi wetu ili waokolewe katika mazingira magumu walionayo, sisi tumejitahidi ingawa bado kuna sehemu tunakwama hivyo ikiongozwa nguvu kutoka serikalini tutapiga hatua kubwa,” amesema.
Pia Mchungaji wa Kanisa hilo, Dk Paul Kaisi amekumbusha kuwa wakati anaanza kutoa huduma katika eneo hilo la Uwanja wa Fisi alianzia katika varanda ya nyumba ya wageni na baadaye kufanikiwa kupata sehemu ya kuanzisha Kanisa.
“Kulikuwa na wakati mgumu na sasa nashukuru kuwepo hapa na nimefanikiwa kubadilisha baadhi ya tabia hatari ambapo yupo dada mmoja aliyekuwa akifanya shughuli za ukahaba hapa kwa miaka 10 na akabadilika na sasa yupo Ruvuma ameolewa na anaishi vema na familia yake, kubadilisha fikra za mtu si kazi ndogo na haihitaji kutumia nguvu,akili na maarifa na kumtegemea Mungu ndio njia sahihi ya kufanikisha hayo,” amesema
Naye Mchungaji Dk.Leonard Ntibanyiha kupitia kikundi cha kanisa hilo kinachiotwa Sambaza Upendo , Amani Tanzania, ambalo linajukumu la kuhudumia vijana walio katika mazingira magumu, wazee, wajane amesema alipata maono ya kuanzisha jambo hilo mwaka 2018 baada ya kupata ndoto akiwa usingizini.
Katika shughuli hiyo ya kuwategemezi yatima, wajane wazee na vijana wanaoishi katika mazingira magumu walitoa misaada ya nguo, viatu kwa makundi hayo jambo ambalo limepongezwa na Diwani, Nyamwija kutokana na kufanya jambo kwa wahitaji halisi.