*Dk. Biteko asema suala la kuwapa nishati wananchi sio hiari
*Asisitiza miradi ya usafirishaji umeme EAPP kukamilika kwa wakati
*Vyanzo vipya vya umeme kuendelezwa kukidhi mahitaji
NA TERESIA MHAGAMA, NAIROBI
BARAZA la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za
Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of Ministers-COM) limekubaliana
kwa pamoja kuwa na usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya umeme
katika nchi wanachama, ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwapatia
wananchi nishati ya kutosha.
Kukamilika kwa miradi kutoka vyanzo mbalimbali vya umeme, kutawezesha
nchi hizo kusaidiana pale nchi mojawapo inapokuwa na upungufu wa umeme
huku msisitizo ukiwekwa kwenye miradi ya usafirishaji
umeme.(Transmission lines).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.
Doto Biteko Februari 27, 2024 katika Mkutano wa 18 wa Baraza la
Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za
Mashariki mwa Afrika
(EAPP Council of Ministers-COM) ambao unafanyika kwa siku mbili
jijini Nairobi, Kenya.
“ Baraza hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinaungana
kwa ajili ya kuendeleza rasilimali za umeme zilizopo pamoja na kupata
umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na
katika Mkutano huu kila nchi imeonesha utayari kufanya biashara ya
umeme pale kunapokuwa na umeme wa ziada.” amesema Dk.Biteko
Ameeleza kuwa kuna idadi kubwa ya watu katika nchi wanachama wa EAPP,
hivyo inahitajika nishati zaidi kwa ajili ya maendeleo ya watu na
viwanda na ndio maana kila nchi imejikita katika kuendeleza vyanzo
mbalimbali vya umeme ajili ya kujipatia nishati ya uhakika.
Amesema chini ya mfumo wa pamoja wa umeme EAPP kuna miradi mbalimbali
iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kuimarisha upatikanaji wa
nishati katika nchi wanachama akitolea mfano mradi wa ujenzi wa
miundombinu ya umeme wa Kenya-Uganda, Kenya-Ethiopia, Kenya-Tanzania,
Tanzania-Rwanda, Tanzania-Uganda, Tanzania-Burundi na DRC-Burundi.
Amesisitiza kuwa, nchi Wanachama zinapaswa kuhakikisha kuwa miradi
hiyo inakamilika kwa wakati ili kupunguza changamoto za umeme kwani
umeme huo utaweza kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine na
kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika .
Awali, Mwenyekiti wa kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa Nishati
ambaye ni Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Davis Chirchir
amesema lengo la nchi kuwa na mfumo huo ni nchi wanachama 13 kufanya
biashara ya mauziano ya umeme pale kunapokuwa na ziada ya umeme, na
kwamba ili suala hilo liwezekane lazima kuwepo na miumbombinu ya umeme
inayounganisha nchi hizo.
Amesema kuwa, majadiliano ya viongozi hao yamelenga katika kuimarisha
muundo wa umoja huo pamoja na ushirikiano na hii ikijumuisha namna ya
kukabiliana na changamoto mbalimbali za umeme pale zinapojitokeza.
Amesema Kenya tayari inafaidika na mfumo huo wa umeme baada ya
kupokea magawati 200 za umeme kutoka nchini Ethiopia, hivyo kuongeza
kiasi cha umeme katika nchi hiyo.
Ameongeza kuwa, takriban watu milioni 600 bado hawajapata nishati ya
umeme barani Afrika kati ya watu takriban Bilioni 1.5 na hii ikionesha
jinsi nguvu zaidi inavyohitajika ili kuwa na nishati ya kutosha kuweza
kukidhi mahitaji.
Nchi Wanachama wa Umoja wa EAPP ni pamoja na Kenya, Tanzania, Sudan
Kusini, Sudan, Uganda, Somalia, Libya, Ethiopia, Misri, Djibouti,
Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia
na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).
Viongozi wengine wanaoshiriki Mkutano huo kutoka Tanzania ni Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi
Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
Mhandisi Gissima Nyamohanga.