NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema kuwa mgao wa umeme unaoendelea hivi sasa nchini unatokana na mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko ule unaozalishwa kwa sasa.
Mramba amesema hayo leo februari 22,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu kuhusu ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan katika nchi ya Norway, Vatican na Addis Ababa, Ethiopia.
Amesema ni kweli kwamba kupitia bwawa la Mwalimu Nyerere wanatarajia kumaliza tatizo hilo la uhaba wa umeme nchini na kwamba wapo katika hatua za mwisho kukamilisha jambo hilo kwa sababu wana mitambo miwili ambayo inatarajiwa kukamilika muda wowote kuanzia sasa.
“Mtambo wa mwanzo umeshafanyiwa majaribio yote na yamekwenda vizuri, kilichobaki ni utaratibu wa kuweza kuingiza umeme wake kwenye gridi ya Taifa ili wananchi waanze kuupata, hivyo muda wowote utaingia kwenye gridi na utaweza kuingiza Megawati 235,” amesema na kuongeza
“Mahitaji ya umeme nchini ni kati ya megawati 300 hadi 400, mfano mpaka leo asubuhi mahitaji ya umeme yalikuwa megawati 304, kwahiyo ukiingiza megawati 235 utaona ni kwa kiasi gani unapunguza uhaba wa umeme uliyokuwepo, zaidi ya asilimia 80 hilo tatizo litakuwa limetibiwa, Unaweza kuamka asubuhi kesho au kesho kubwa unakuta mgao wa umeme hakuna kabisa,” amesema