*Yawafunda nidhamu ya fedha
*Yazindua shindano kwa Waandishi wa Habari Chipukizi wa Habari za biashara, fedha na Uchumi
*Yawaandalia Siku ya Vyombo vya Habari
*Yawapa tuzo Waandishi Nguli
*Wamo Edda Sanga na Ndimara Tegambwage
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI ya CRDB imeendesha semina maalumu kwa wadau wa sekta ya habari nchini ‘CRDB Bank Media Day’ iliyofanyika katika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es salaam.
Semina hiyo ni mwendelezo wa jitihada za CRDB kutambua mchango wa sekta ya habari nchini.
Semina hiyo inafanyika kwa mara ya pili mfululizo ambapo ilianza rasmi mwaka 2023.
Akifungua semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema “CRDB Bank Media Day” ya mwaka huu imejikita katika kuangazia ripoti ya Finscope 2023 na namna gani vyombo vya habari vinaweza kuchochea ujumuishi nchini.
“Ripoti ya Finscope ya 2023 inaonesha ujumuishi wa kibenki upande wa huduma za benki ni asilimia 22 pamoja na jitihada na ubunifu mkubwa katika bidhaa.
“Hii inaonesha kuna ombwe kubwa la elimu ya fedha, hivyo leo tumepata kujadili ninamna gani wenzetu wa sekta ya Habari wataweza kusaidia kutoa taarifa na huduma za fedha,” ameeleza Nsekela.
Katika semina hiyo waandishi wa habari walipata fursa ya kupata mafunzo ya namna ya bora ya kaandaa na kutoa mafunzo ya taarifa za biashara, fedha na uchumi. Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo katika kusaidia kujenga waandishi mahiri nchini.
Katiak hatuna nyingine, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo iliyowaleta wadau wa sekta ya habari kujadili namna ya kuongeza mchango wake katika maendeleo hususani katika kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini. Matinyi amewahakikishia wadau wa sekta hiyo kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri yatakayosaidia kuboresha sekta ya habari.
Mada mbalimbali zimewasilishwa katika semina hiyo ikiwamo ‘Jukumu la Vyombo vya Habari katika kuchochea Ujumuishi wa Kifedha’ iliyowasilishwa na Mhariri Mstaafu wa National Media Group Kenya, Charles Onyango ‘Elimu ya Fedha kupitia Mitandao ya Jamii’ iliyowasilishwa na Fayness Sichalwe mshauri wa masuala binafsi ya fedha na Mwanzilishi wa Personal Finance Hub, na Usomaji na Uwasilishaji wa Taarifa za Fedha’ iliyowasilishwa na Dk. Ndalahwa Masanja, Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha ESAMI.
Katika Semina hiyo iliyohudhuriwa na waandishi na wahariri kutoka vyombo mbali nchini, Benki ya CRDB pia imezindua shindano maalumu la kutafuta waandishi wahabari wachanga wa habari za biashara, fedha, na uchumi. Shindano hilo ambalo litaendeshwa kwa muda wa miezi miwili hadi Aprili 12 2024, litatoa washindi watatu ambao watajishindia zawadi ya Sh. Milioni Moja na nafasi ya kufanya kazi na Benki ya CRDB.
Aidha, katika hafla hiyo Benki ya CRDB imetoa tuzo za kutambua mchango wa waandishi wa habari wawili nguli katika sekta ya habari nchini.
Waliokabidhiwa tuzo hizo ni Edda Sanga Mwandishi mstaafu wa Shirika la Habari la Tanzania (TBC) na Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), na Ndimara Tegambwage mwandishi wa zamani wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, na moja ya waanzilishi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA).