NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania na Poland zimekubaliana kushirikiana katika maeneo sita ambayo ni kilimo, afya, elimu, uwekezaji, utalii, biashara Tehama,
Aidha amesema wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano uliyopo baina ya nchi mbili na kuhamasisha uwekezaji zaidi kwenye sekta za kimkakati kama vile viwanda, uzalishaji, nishati, madini, gesi asilia na Uchumi wa buluu
Rais Samia ameyasema hayo leo Januari 9,2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza mazungumzo baina yake na Rais wa Poland Andrzeja Duda ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku mbili.
Aidha amesema amemshukuru Rais Duda kwa utayari wa nchi yake kupitia Wakala wa Mikopo ya Usafirishaji (Kuke) kutoa bima kwa benki za biashara kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa vipande vya Makotopola hadi Tabora na Tabora hadi Isaka Zambia.
Hata hivyo amesema ziara hiyo ni kielelezo cha kuendelea kuimarika kwa urafiki na ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na Poland ambao umekuwepo tangu mwaka 1962.
“Poland ni mbia wetu mkubwa sana katika bara la Ulaya kwani ni miongoni mwa nchi 10 ambazo raia wake utembelea Tanzania kwa wingi, kwa madhumuni ya utalii, lakini pia imekuwa ikichangia shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini ikiwemo sekta ya afya,” amesema na kuongeza
“Poland wamechangia utoaji huduma katika hospitali tano hapa nchini ambapo ndani ya mkoa wa Dar es slaam ipo hospitali ya Aga Khan, kituo cha afya Chanika, hospitali ya Rufaa mkoa wa Temeke, Mwananyamala na Nyamagana iliyopo jijini Mwanza,”
Naye Rais wa Poland, Andrzeja Duda amesema nchi yake inawakaribisha vijana wa Kitanzania Kwenda nchini Poland ili kupata elimu kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo teknolojia ya uchimbaji madini.
Rais Duda amesema nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania ambao umedumu kwa takribani miaka 62 na kwamba wapo tayari kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na viwanda pamoja na uzalishaji kwa kutumia teknolojia za kisasa.
“Tutashawishi wawekezaji wengi zaidi ambao baadhi yao wapo tayari barani Afrika kuja kuwekeza hapa Tanzania ili kuweza kuongeza tija kwenye malighafi zinazopatikana Tanzania,” amesema Rais Duda