NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha madini yanayozalishwa hapa nchini yanaongezewa thamani ndani ya Tanzania ili kukuza uchumi wa viwanda, kuongeza ajira, kuimarisha mapato ya Taifa na kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na rasilimali hizo kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Hayo yameelezwa leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi leo Novemba 19, 2026 wakati akifungua Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TMIC 2026), jijini Dar es Salaam, ambapo amesema Tanzania imejielekeza katika kuimarisha viwanda vya ndani vya uchenjuaji, usafishaji, uyeyushaji na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na madini ili kupunguza utegemezi wa kuuza madini ghafi.
Amesema nchi nyingi za Afrika bado hazijanufaika kikamilifu na utajiri wa rasilimali madini kutokana na uhaba wa viwanda vya kuongeza thamani, hivyo Tanzania imeendelea kuboresha sera, sheria na kanuni ili kuvutia uwekezaji na kuunganisha sekta ya madini na viwanda, nishati na kilimo.
Katika hatua nyingine, Ndejembi amesema Serikali imeridhia kutenga asilimia 10 ya mapato ya madini kwa ajili ya kufadhili utafiti wa rasilimali mpya kupitia Mfuko wa Utafiti wa Madini (Minerals Survey Fund), huku akiielekeza Wizara ya Madini kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa kikamilifu na kutumika kwa kile kilichokusudiwa.
Aidha, ameitaka Wizara kuhakikisha wawekezaji wanatekeleza masharti ya leseni zao kwa wakati na kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo, ambao wanachangia zaidi ya asilimia 40 ya mapato yatokanayo na shughuli za madini.
Katika kutambua mchango wake katika kuimarisha usimamizi, mageuzi na maendeleo ya Sekta ya Madini nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa tuzo maalum ya kutambua uongozi wake na jitihada zake katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza thamani ya madini na kuhakikisha rasilimali hizo zinachangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi.
Akielezea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa ajenda hiyo, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Sekta ya Madini imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi, ikichangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, huku mauzo ya madini nje ya nchi yakifikia Dola za Marekani bilioni 5.4, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 13.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha viwanda vya kuongeza thamani madini, ikiwemo viwanda 8 vya kusafisha dhahabu, viwanda 16 vinavyoendelea kujengwa kwa ajili ya kuchakata madini ya kimkakati kama nickel na shaba, pamoja na miradi ya uchakataji wa madini tembo na Ferro-Niobium.
Katika kuimarisha akiba ya Taifa, Mavunde amesema Tanzania imefanikiwa dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayofikia tani 39.6, na hivyo kuingia miongoni mwa nchi tano za Afrika zenye akiba kubwa ya dhahabu kupitia Benki Kuu zao.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo kupitia ajira, utoaji wa bidhaa na huduma, pamoja na fursa za uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.
Akizungumzia mkutano huo, Waziri Mavunde amesema TMIC 2026 umekutanisha zaidi ya washiriki 1,715 kutoka ndani na nje ya nchi, ukiwa jukwaa muhimu la kuimarisha diplomasia ya uchumi, kuvutia uwekezaji na kujadili fursa za kuongeza thamani madini.
Mkutano huo unafanyika kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, ukiwa na kaulimbiu isemayo “Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi.”

