FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, ameitaka sekta ya fedha kuimarisha upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha kwa wanawake na vijana ili kuwawezesha kupata mitaji, kukuza biashara na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Amesema ujumuishi wa kifedha haupaswi kupimwa kwa idadi ya watu wenye akaunti za benki au laini za simu pekee, bali pia kwa upatikanaji wa huduma hizo, uwezo wa kuzitumia kukuza biashara na kuboresha maisha pamoja na gharama nafuu za huduma hizo.
Akizungumza leo, Novemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, katika kilele cha Mkutano wa Ujumuishi wa Kifedha kwa Wanawake na Vijana pamoja na uzinduzi wa ripoti ya ujumuishi wa kifedha, Luswetula amesema wajasiriamali wanawake na vijana bado wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mikopo kutokana na masharti magumu, ukosefu wa dhamana, gharama kubwa za huduma za kifedha na uelewa mdogo wa teknolojia za kidijitali.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) itaendelea kuchambua mapendekezo ya ripoti hiyo ili kubaini hatua za kisera na kiutendaji zitakazosaidia kuondoa vikwazo hivyo, ikiwamo kukamilisha kanuni za matumizi ya mali zinazohamishika kama dhamana ya mikopo.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), Mercy Silla, amesema ripoti hiyo imebainisha mapendekezo saba ya kuboresha huduma za kifedha, yakiwamo kuongeza uwazi wa masharti ya mikopo, kulinda wakopaji, kurahisisha huduma kwa wasio na vitambulisho na kuongeza mawakala wa huduma za kifedha vijijini.
Amesema mapendekezo mengine ni kuweka mfumo wa kutumia mali zinazohamishika kama dhamana ya mikopo, kuimarisha mifumo ya malipo inayounganishwa na kuweka kipimo cha pamoja cha kufuatilia ujumuishi wa kifedha kwa kuzingatia jinsia, umri, eneo na sekta.
Ameeleza kuwa TWCC imekuwa ikitekeleza programu za kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa miaka 21 na inatarajia mapendekezo ya ripoti hiyo yafanyiwe kazi ili kuleta mabadiliko katika upatikanaji wa huduma za kifedha badala ya kubaki kwenye maandishi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Dk. Mwajuma Hamza, amesema taasisi hiyo imekuwa ikiendesha programu za kuwawezesha wanawake kupata mitaji na kushiriki katika shughuli za kiuchumi, huku ikianzisha idara maalumu ya vijana baada ya kubaini changamoto za ajira zinazowakabili.
Amesema utafiti umeonesha Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya huduma za kidijitali za kutuma na kupokea fedha, hata hivyo urasimishaji wa biashara bado ni muhimu ili kuwawezesha wajasiriamali kunufaika na mikopo ya benki na mifuko ya uwezeshaji.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Jabiri Makame, amesema Baraza hilo litaendelea kuratibu taasisi mbalimbali za Serikali katika kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo ili kuimarisha ujumuishi wa kifedha kwa wanawake na vijana.
Amesema ajenda hiyo ni muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, ikiwamo kujenga uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza wastani wa kipato cha Mtanzania hadi dola 7,000 kwa mwaka.

