NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
LICHA ya Afrika kuwa miongoni mwa Mabara yenye utajiri mkubwa wa madini muhimu duniani, mamilioni ya wananchi wake bado wanaendelea kuishi katika umasikini, hali ambayo imeelezwa kuwa haiwezi kuendelea kuvumiliwa katika kizazi hiki cha mabadiliko ya kiuchumi duniani.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Aprili 27,2026 na Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn Boshe wakati akifungua Kongamano la Kikanda kuhusu matumizi ya madini muhimu ya Afrika kwa ajli ya kukuza viwanda lililofanyika katika makao makuu ya Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi Barani Afrika (UNECA) jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Boshe amesema ni jambo la kushangaza kuona bara lenye utajiri mkubwa wa madini muhimu kama cobalt, lithium, copper, manganese na madini adimu likiendelea kushuhudia wananchi wake wakikosa kunufaika na rasilimali hizo.
Amesema mahitaji ya madini hayo yameongezeka kwa kasi duniani kutokana na matumizi yake katika utengenezaji wa betri, magari ya umeme na mifumo ya nishati jadidifu, lakini Afrika bado haijafaidika ipasavyo kwa sababu imeendelea kubaki katika nafasi ya kuuza malighafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani.
Amesema hali hiyo imeifanya Afrika kuendelea kuwa chanzo cha malighafi kwa mataifa yaliyoendelea huku faida kubwa ya uchumi ikibaki nje ya bara hilo.
“Mpito wa uchumi wa kijani haupaswi kuwa sura nyingine ya uchimbaji wa rasilimali bila mabadiliko ya kiuchumi kwa Waafrika. Lazima tubadili mwelekeo huu na kuhakikisha madini yetu yanakuwa msingi wa maendeleo ya viwanda na ustawi wa wananchi wetu,” amesema.
Amesisitiza kuwa Afrika inapaswa kuwekeza katika viwanda vya kusafisha na kuchakata madini, pamoja na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na madini hayo ili kuongeza ajira, mapato na ushindani wa kiuchumi.
Aidha, amesema maendeleo ya viwanda hayawezi kufikiwa bila uwekezaji mkubwa katika miundombinu ikiwemo nishati, reli, barabara na maeneo maalumu ya viwanda yatakayorahisisha biashara na kuvutia wawekezaji.
Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda kupitia African Continental Free Trade Area (AfCFTA), akieleza kuwa nguvu ya pamoja ya Afrika inaweza kujenga mnyororo kamili wa thamani wa madini na bidhaa za teknolojia ya kijani.
Kwa upande mwingine, amezitaka serikali za Afrika kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na ulinzi wa maslahi ya wananchi pamoja na mazingira.
Desalegn ameweka wazi kuwa wakati umefika kwa Afrika kuacha kuwa msambazaji wa malighafi na badala yake kuwa kitovu cha viwanda vya kisasa, akisema huo ndio njia pekee ya kuondoa umaskini na kujenga ustawi wa kweli kwa wananchi wa bara hilo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Tanzania, Msafiri Mbibo amesema Afrika ina nafasi kubwa ya kutumia utajiri wa madini muhimu kuchochea maendeleo ya viwanda vya kijani na maendeleo endelevu, huku akisisitiza usimamizi bora wa rasilimali hizo ili wananchi wanufaike.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Mbibo amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini na sekta hiyo imeendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira, kipato na maendeleo ya wananchi, huku ikiwa na uwezo wa kusaidia kupunguza umasikini katika jamii.
Mbibo ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa uwajibikaji kwa kuzingatia ustawi wa jamii, ulinzi wa mazingira pamoja na kuimarisha ushiriki wa Watanzania kupitia sera za kuongeza thamani ya madini.
Aidha, amesema pamoja na fursa zilizopo, bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo uchimbaji haramu, uharibifu wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kutafuta suluhisho la changamoto hizo.
Mbibo amesema Tanzania inaendelea kutafuta ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kubadilishana uzoefu na kutumia teknolojia za kisasa katika sekta ya madini kwa lengo la kuongeza ufanisi, kulinda mazingira na kukuza maendeleo ya viwanda barani Afrika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo ameeleza kuwa Afrika ipo katika hatua muhimu inayohitaji uongozi thabiti, sera bora na usimamizi makini wa rasilimali, hususan madini mkakati, ili kuchochea ukuaji wa viwanda, ajira na uchumi wa kijani.
Singo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza maendeleo endelevu na kuimarisha uongozi barani Afrika huku akipongeza ushirikiano unaoendelea kati ya taasisi hiyo na wadau wa kimataifa, akibainisha kuwa umekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza mijadala ya kisera, kuimarisha taasisi na kukuza maendeleo jumuishi barani Afrika.
“Tunathamini ushirikiano tuliojenga na tunaendelea kushukuru kwa msaada wa wadau wetu. Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya kuunda mustakabali wa maendeleo ya Afrika kupitia mazungumzo yenye tija na ushirikiano,” amesema Singo.
Ameipongeza Serikali ya Ethiopia kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo pamoja na kuwezesha ushiriki wa wadau mbalimbali wakiwemo vijana, watunga sera, sekta binafsi na asasi za kiraia, akisisitiza kuwa ushirikishwaji wa makundi yote ni muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu.




