NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
TAASISI ya Uongozi kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi Barani Afrika (UNECA), itafanya kongamano la kikanda lenye dhima ya Kuimarisha usimamizi wa madini mkakati kwa ajili ya viwanda vya kijani na maendeleo endelevu barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Taasisi hiyo,kongamano hilo ni tukio muhimu litakalofanyika kabla ya Mkutano wa 12 wa Kikanda wa Maendeleo Endelevu, unaoratibiwa na UNECA.
Aidha kongamano hilo litajadili masuala ya usimamizi wa madini mkakati, ikiwemo mikakati ya kisera, uwezo na fursa; na kutoa mapendekezo ya namna ya kuongeza thamani, kuchochea viwanda vya kijani na kuimarisha tabianchi.
“Kongamano litafanyika Aprili 27, 2026 huko Makao Makuu ya UNECA, Addis Ababa, Ethiopia, Mgeni Rasmi wa kongamano anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Hailemariam Dessalegnd” imeeleza taarifa hiyo
Imesema kuwa Wasilisho kuu litatolewa na Dk. Paul Jourdan, Mchambuzi Sera wa Madini anayejitegemea.Washiriki wengine ni viongozi waandamizi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na sekta zote ikiwemo sekta ya umma, sekta binafsi, sekta ya elimu ya juu, na sekta ya asasi za kiraia.
“Kongamano litajumuisha ufunguzi, mijadala ya jopo, mawasilisho ya kitaalamu,na mjadala wa kupaza sauti za vijana, wanawake, na jamii katika mada husika,” imeeleza
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa Kongamano hilo linalenga pia kutoa fursa ya kujadili namna ya kuhakikisha usimamizi madhubuti wa madini mkakati ili kuchochea viwanda vya kijani na maendeleo endelevu barani Afrika.
“Malengo mahususi ni Kuimarisha uelewa wa usimamizi wa madini mkakati barani Afrika, ikiwemo mikakati ya kisera, kwa kutumia mifano ya sasa na ile ya zamani, Kuainisha namna bora ya kuchimba madini mkakati na kuimarisha mnyororo wa thamani barani Afrika ili kuchochea viwanda vya kijani na maendeleo jumuishi pamoja na kujadili na kupendekeza miongozo inayozingatia usawa baina ya uchimbaji madini na utunzaji mazingira, pamoja na maslahi na haki za jamii,” imeeleza

