NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WATAALAM wa Wizara ya Madini wakiongozwa na Katibu Mkuu,Mhandisi Yahya Samamba, wamekutana kujadili mwelekeo wa mpango mkakati unaolenga kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa. Kikao hicho kilijikita katika kubaini maeneo yenye tija kubwa, ikiwemo uongezaji thamani wa madini, uwekezaji wa teknolojia, na uboreshaji wa mazingira ya uchimbaji na biashara ya madini.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Aprili 21, 2026, Jijini Dodoma Mhandisi Samamba alisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa rasilimali madini, akieleza kuwa mpango huo unapaswa kuendana na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050 kwa kuhakikisha sekta inakuwa shindani kimataifa na yenye manufaa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dk. AbdulRahman Mwanga alieleza kuwa utekelezaji wa mikakati hiyo utaongeza uwazi, tija, na mapato ya Serikali kupitia udhibiti imara wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Menejimenti ya Wizara imeazimia kuimarisha uratibu kati ya taasisi za sekta, kuongeza ushirikishwaji wa sekta binafsi, na kuharakisha mageuzi ya kisera na kisheria ili kuwezesha ukuaji endelevu wa sekta ya madini nchini.





