MBEYA,TANZANIA
JUMATANO MACHI 26,2026
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Serikali za Mitaa (Halmashauri) imeendelea kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyohusiana na uchakachuzi wa mbolea nchini kwa kuweka mifumo imara ya ukusanyaji na upashanaji wa taarifa pale vitendo hivyo vinapojitokeza.
Uchakachuzi wa mbolea ni hujuma kubwa inayodhoofisha juhudi za wakulima na kuathiri uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Joshua Ng’ondya ,Meneja wa Kanda,Nyanda za Juu Kusini Serikali haitavumilia vitendo hivyo na imejipanga kuhakikisha vinakomeshwa kabisa.
Aidha Meneja huyo wa Kanda ameeleza kuwa,Katika kuhakikisha udhibiti madhubuti, TFRA imeanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa wafanyabiashara wanaotiliwa mashaka kwa kuchunguza mwenendo wa mauzo yao ya mbolea ili kubaini ukiukwaji wa Sheria na Kanuni.
“Mamlaka imeweka mtandao mpana wa wasiri katika maeneo mbalimbali nchini ambao hutoa taarifa kwa wakati kuhusu vitendo vya uchakachuzi wa mbolea na ukiukwaji mwingine wa Sheria ya mbolea
“Hatua hii imewezesha kuchukuliwa kwa hatua za haraka dhidi ya wahusika, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya dola na kuwatoza faini kali kwa mujibu wa sheria na Kanuni
“TFRA inatoa wito kwa wafanyabiashara wote wa mbolea kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo ikiwemo ya utekelezaji wa mpango wa ruzuku.” amefafanua Meneja huyo
Katika hatua nyingine Meneja huyo amesema Mamlaka inaonya kuwa ukiukwaji wowote utachukuliwa kwa uzito mkubwa, na wahusika watachukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwafungulia mashitaka yakiwemo ya uhujumu Uchumi.
Kwa upande wa wakulima, Meneja huyo amekwenda mbali zaidi kwa kuwasihi wakulima kununua mbolea kupitia mfumo rasmi wa usambazaji wa mbolea.
“Ununuzi wa mbolea nje ya mfumo huo huongeza hatari ya kupata mbolea isiyo na ubora na kuchochea vitendo vya uhalifu.” amesisitiza
Amesema kuwa, Serikali inasimamia ubora wa mbolea kuanzia inapowasili nchini hadi inapomfikia mkulima, hivyo ni muhimu kufuata utaratibu uliowekwa.
” Wakulima na wananchi kwa ujumla wanahimizwa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika wanapobaini vitendo vya uuzaji wa mbolea nje ya mfumo rasmi au uchakachuzi, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.”amejinasibu Meneja huyo wa FRA
TFRA inasisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara waadilifu pamoja na wananchi katika kupambana na vitendo hivi viovu.
Sambamba na hayo yote,ametanabaisha kuwaMamlaka itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuzuia uingizwaji na usambazaji wa mbolea zisizo halali.
“Mamlaka inaamini kuwa ushirikiano wa pamoja na uimarishaji wa mifumo ya utoaji taarifa ni nguzo muhimu katika kutokomeza hujuma za mbolea nchini.” amehitimisha Meneja huyo

