NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, Fadhili Mitimingi, amesema kupitia ushirikiano kati ya Serikali na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Watanzania wengi wamepata fursa ya kusoma na kupata mafunzo nje ya nchi, jambo ambalo limechangia kuongeza ujuzi na utaalamu katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini.
Mtimingi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Utumishi katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Watanzania waliosoma nchini Japan na kaika nchi nyingine kwa ufadhili wa Serikali ya Japan (JATA).
Amesema mara nyingi watanzania wanaopata fursa ya mafunzo kupitia JICA wanaporejea nchini hutumia ujuzi walioupata kuanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kueneza maarifa hayo kwa watu wengine katika jamii.
“Miradi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhamasisha matumizi ya mbinu bora na za kisasa katika sekta muhimu za uzalishaji,” amesema
Aidha Mitimingi amesema kuwa umoja wa JATA unaisaidia Serikali kupata wataalamu wenye uwezo wa kuleta matokeo chanya katika jamii hususan kwa kutumia teknolojia na mbinu za kisasa kwenye sekta za kilimo, ufugaji pamoja na miundombinu.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mikami Yoichi amesema katika mkutano huo kulikuwa na wawasilishaji watatu ambao walieleza kuhusu miradi mbalimbali waliyoitekeleza hadi sasa na kwamba miradi yote iliyowasilishwa ilikuwa ya kuvutia na ya kutia moyo, huku baadhi yake ikiwa tayari imeanza kuonyesha matokeo halisi.
Mwakilishi Mkazi wa JICA Tanzania, Ara Hitoshi amesisitiza kuwa lengo kuu la mafunzo wanayoyatoa ni kuchangia maendeleo ya Tanzania na kwamba ili kufanikisha jambo hilo, ni muhimu kwa washiriki wanaporudi kutoka kwenye mafunzo, kuchukua hatua mbalimbali za kusaidia wengine kwa kutumia maarifa na uzoefu walioupata.
Amesema katika kufanikisha hilo ushirikiano na mawasiliano kati ya washiriki wa mafunzo hayo unahitajika kwami ni jambo la muhimu huku akibainisha kuwa JICA pia linaendelea kuunga mkono juhudi hizo.
“Kwa sababu hiyo,ninaamini kuwa nafasi na jukumu la JATA ni muhimu sana. Natarajia kuona chama hiki kinaendelea kuwa hai zaidi ili kila mshiriki aliyepata mafunzo nchini Japan aweze kutumia maarifa aliyoyapata na hivyo kuchangia maendeleo ya Tanzania,” amesema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JATA, Gregory Mlay amesema kuwa JATA kumejaa wataalamu kutoka sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, mifugo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), biashara pamoja na afya.
Amesema wataalamu hao wamejipanga kukusanya nguvu zao kwa pamoja ili kuwasaidia wananchi kwa kushirikiana katika miradi ya maendeleo na kutoa utaalamu wao katika maeneo mbalimbali.
Aidha, amesema Mkutano Mkuu wa JATA umekutanisha kada tisa tofauti za wataalamu ambao kwa pamoja wanajadili mafanikio yaliyopatikana hadi sasa pamoja na kupanga mipango ya utekelezaji wa shughuli nyingine za maendeleo.
“Mkutano huu pia utatumika kupanga mikakati ya pamoja itakayosaidia kuendeleza shughuli za JATA na kuchangia maendeleo ya jamii,” amesema.
Ameongeza kuwa miongoni mwa mikakati mipya ya maendeleo ya JATA ni kuongeza juhudi katika masuala ya utunzaji wa mazingira, maendeleo ya mifugo na ufugaji, kilimo cha kisasa pamoja na kuboresha sekta ya afya ili kuchangia ustawi wa jamii.
Katika hatua nyingine, mmoja wa wanufaika wa programu za mafunzo hayo, Godfrey Christopher, amesema kupitia mradi huo waliweza kujifunza mbinu mbalimbali za kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi na kuboresha maisha yao.
Amesema elimu hiyo imewasaidia kuelewa namna ya kusindika na kuhifadhi mazao ya uvuvi kwa kutumia teknolojia bora,jambo ambalo linasaidia kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza thamani yake sokoni.
Ameongeza kuwa ujuzi huo utaendelea kusambazwa kwa jamii ili wavuvi na wananchi wengine waweze kunufaika na rasilimali zilizopo kwa njia endelevu na yenye tija zaidi.



