NA MWANDISHI WETU,TEMEKE,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeonesha upendo na mshikamano kwa jamii inayowazunguka kwa kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Sandali iliyopo Kata ya Sandali, Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho kuelekea ya Siku ya Wanawake Duniani.
Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo, Ofisa Tawala wa TFRA, Ruth Magesa, amesema ziara hiyo imelenga kuonesha upendo kwa watoto wenye changamoto ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Amesema kuwa, TFRA inatambua mchango mkubwa wa walimu na walezi wanaohudumia watoto hao na kueleza kuwa kama sehemu ya uwajibikaji wa Mamlaka kwa jamii inayowazunguka imepanga kusaidia katika kukarabati kisima cha maji katika shule hiyo ili kuboresha mazingira ya wanafunzi hao.
Akizungumza leo Machi 5, 2026 Diwani wa Kata ya Sandali, Mrisho Kamba ameipongeza TFRA kwa kuguswa na mahitaji ya watoto hao na kueleza huduma iliyotolewa na Mamlaka hiyo umeleta faraja na kuwatia moyo walimu, walezi na jamii inayowazunguka watoto hao.
Akizungumza kwa niaba ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sandali,Rose Lwellengele ameishukuru TFRA kwa msaada huo akisema changamoto zinazowakabili watoto wenye mahitaji maalum ni nyingi, hivyo kitendo cha taasisi hiyo kufika shuleni hapo na kutoa msaada ni faraja kubwa kwao.
Naye Subira Mwandeka, mtaalam wa kufundisha watoto wenye ulemavu wa akili na usonji, amesema kitengo hicho kilianzishwa mwaka 2019 ambapo walifanya uhamasishaji katika ngazi za serikali za mitaa kwa kutembelea nyumba kwa nyumba kutoa elimu kwa jamii ili kuwapa fursa Watoto wenye mahitaji maalum kupata elimu kama wanavyopata watoto wenye hali za kawaida.
Amesema juhudi hizo zimewezesha watoto wengi wenye mahitaji maalum kuanza kuhudhuria shule na walimu wanaendelea kufuatilia maendeleo yao hata majumbani ili kuhakikisha wanapata msaada na kukubalika katika jamii.
Naye mlezi wa watoto hao, Mariam Maingwa, amesema watoto wenye mahitaji maalum wanahitaji uangalizi na msaada mkubwa kutoka kwa jamii, hivyo ametoa shukrani kwa TFRA kwa kuonesha moyo wa kujali na kuahidi kuwa ushirikiano kati ya walimu, walezi na wadau utaendelea ili kuwasaidia watoto hao kupata malezi na elimu bora.








