NA MWANDISHI WETU,PWANI
WIZARA ya Biashara kupitia Idara ya Viwanda imewataka wamiliki wa viwanda na wazalishaji wa bidhaa mkoani Pwani kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne,Februari 10,2026 na Ofisa Biashara na Uwekezaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Rehema Akida kwenye mkutano wa wadau na wamiliki wa viwanda uliofanyika mkoani Pwani, uliolenga kuhamasisha usajili wa nembo hiyo ya Made in Tanzania, mkutano ulioandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
Pia Akida amewataka wazalishaji na wamiliki hao wa viwanda kutumia Nembo ya Bidhaa na Huduma (Made in Tanzania) katika bidhaa na huduma zao, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kutambulisha bidhaa hizo kitaifa na kimataifa pamoja na kuziongezea thamani kibiashara.
Amesisitiza kuwa bidhaa zinazopata nembo hiyo hupata fursa kubwa ya kupenya katika masoko ya kimataifa kutokana na utambulisho wake rasmi, huku akibainisha kuwa bidhaa nyingi zinazozalishwa nchini zinapendwa na kufahamika kutokana na uasilia na ubora wake.
“Bidhaa za Tanzania zina sifa ya kipekee na zinathaminiwa kwa uasilia wake. Ni wajibu wa Watanzania kujivunia bidhaa zao na kuchukua hatua ya kuzitambulisha rasmi kwa kutumia nembo ya Made in Tanzania,” amesema Akida.
Ameongeza kuwa matumizi ya nembo hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kukuza uzalishaji wa ndani, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia viwanda na biashara
Aidha Akida amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade kwa kutambua mchango wa Mkoa wa Pwani kama miongoni mwa mikoa yenye wazalishaji wakubwa wa viwandani nchini na kuanza kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa bidhaa zao kuwa na nembo hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Ujengaji Uwezo na Huduma za Ushauri kutoka TanTrade, Boniface Mrema,amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikifanya kazi bega kwa bega na sekta binafsi, wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kufungua masoko, kuimarisha ushindani na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya kitaifa na kimataifa.
Mrema amesema Mkoa wa Pwani ni kituo muhimu cha uzalishaji na miundombinu ya masoko, hivyo amewaalika wamiliki wa viwanda na wazalishaji kutumia nembo ya Made in Tanzania kama chombo cha kimkakati cha kutofautisha bidhaa za Watanzania sokoni, kujenga imani kwa walaji, kulinda chapa dhidi ya bidhaa feki na kuongeza fursa ya kuuza bidhaa katika masoko ya Afrika Mashariki, Agoa na SADC.
Ametoa wito kwa wazalishaji kujisajili na kuomba matumizi ya nembo hiyo kwa bidhaa zilizokidhi viwango, kuboresha ubora na vifungashio, kushirikiana na TanTrade katika kupata masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kujengewa uwezo wa kibiashara ili kufungua milango ya masoko ya kikanda na kimataifa.
Naye mmiliki wa kiwanda cha Animal Care Company Ltd, kinachojishughulisha na uzalishaji wa vyakula vya mifugo, vifaranga na uuzaji wa mayai, Iddy Nasibu amesema wamevutiwa na nembo ya Made in Tanzania akieleza kuwa ni jukwaa zuri kwa wafanyabiashara kuwa sehemu ya wazalishaji wa bidhaa zinazoweza kushindana kimataifa.
Ameishukuru TanTrade kwa kuahidi kushirikiana na wafanyabiashara katika safari za maonesho na mikutano ya kibiashara, jambo litakalosaidia kukuza uwezo wao wa uzalishaji hususan katika kuhakikisha ubora wa bidhaa zao.
Kwa upande wake,Mboka Mwampyate, msindikaji wa juisi na unga wa mhogo, amesema nembo ya Made in Tanzania ni fursa muhimu itakayowasaidia kukuza bidhaa zao, kuongeza thamani na kufanya biashara kwa kujiamini zaidi katika masoko mbalimbali.






