NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kubakiza Riba ya Benki Kuu (CBR) katika kiwango cha asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026, hatua inayolenga kudumisha utulivu wa bei na kuendelea kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kilichofanyika Januari 7,2026 baada ya tathmini kuonesha kuwa mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.
Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema kubakiza CBR katika kiwango kilekile kilichokuwepo robo ya nne ya mwaka 2025 kutasaidia kuimarisha mazingira ya mikopo, kuongeza uwekezaji na kuhakikisha ukuaji wa uchumi unabaki katika kiwango cha kuridhisha.
Kwa kuzingatia uamuzi huo, BoT itaendelea kutekeleza sera ya fedha kwa kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki (7-day interbank rate) inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.
Aidha Tutuba amesema Kamati ya Sera ya Fedha imeeleza kuwa uchumi wa dunia uliendelea kuimarika kwa kasi ya wastani mwaka 2025 licha ya changamoto za ongezeko la ushuru wa forodha, migogoro ya kisiasa na hali ya kutokutabirika kwa masoko ya dunia.
Amesema Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linakadiria ukuaji wa uchumi wa dunia kufikia asilimia 3.2 mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 3.3 mwaka 2024, huku kasi hiyo ikitarajiwa kuendelea hadi mwaka 2026.
“Mfumuko wa bei duniani umeendelea kupungua kutokana na kushuka kwa bei za nishati na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha katika nchi nyingi, hali ambayo inatarajiwa kuendelea kusaidia mfumuko wa bei nchini kubaki ndani ya lengo mwaka 2026.
“Kwa upande wa bei za mafuta ghafi, Kamati imebaini kuwa zilishuka hadi kufikia kati ya dola 62 hadi 65 kwa pipa katika robo ya nne ya mwaka 2025, na zinatarajiwa kubaki katika viwango hivyo robo ya kwanza ya mwaka 2026. Hali hiyo inatarajiwa kupunguza shinikizo la mfumuko wa bei na mahitaji ya fedha za kigeni, hivyo kuimarisha utulivu wa thamani ya shilingi,” Amesema Tutuba
Wakati huo huo, amesema bei ya dhahabu imeendelea kupanda na kufikia kiwango cha juu cha dola za Marekani 4,421.65 kwa wakia, hali inayotarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuimarisha zaidi thamani ya shilingi ya Tanzania.
Hata hivyo Tutuba amesema tathmini ya uchumi wa ndani imeonesha kuwa uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa kasi ya takriban asilimia 5.9 mwaka 2025, ukichangiwa zaidi na sekta za kilimo, madini na ujenzi.
Aidha amesema kwa upande wa Zanzibar, uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2026, ukichangiwa na ujenzi, utalii na uzalishaji viwandani.
“Hata hivyo Mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka kwa wastani wa asilimia 20.3, huku katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, uchumi wa Tanzania Bara ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6 na Zanzibar kwa asilimia 7.2.
“Mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu, ambapo kwa robo ya nne ya mwaka 2025 ulikuwa asilimia 3.5 kwa Tanzania Bara na asilimia 3.4 kwa Zanzibar. Kamati inatarajia mwenendo huu kuendelea katika robo ya kwanza ya mwaka 2026,” amesema Tutuba
Kuhusu Sekta ya benki, amesema imeendelea kuwa imara ikiwa na ukwasi na mtaji wa kutosha, huku uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) ukishuka hadi asilimia 3.1, chini ya ukomo unaokubalika wa asilimia 5. Mifumo ya malipo nayo imeendelea kufanya kazi kwa ufanisi mijini na vijijini.
“Sekta ya nje imeendelea kuimarika, ambapo nakisi ya urari wa malipo ya kawaida ilipungua hadi asilimia 2.2 ya Pato la Taifa mwaka 2025, kiwango cha chini zaidi katika miaka mitano. Akiba ya fedha za kigeni ilifikia zaidi ya dola bilioni 6.3, sawa na miezi 4.9 ya uagizaji wa bidhaa na huduma, ikiwa juu ya kiwango kinachopendekezwa kimataifa,” Amesema Tutuba
Kwa upande wa sera ya bajeti, Tutuba amesema makusanyo ya kodi yaliendelea kuimarika huku deni la Serikali likibaki kuwa himilivu. Uwiano wa deni la umma kwa Pato la Taifa ulipungua hadi asilimia 40.6 mwaka 2024/25, chini ya ukomo wa kimataifa wa asilimia 55.




