NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAAJIRIWA wapya wa Tume ya Madini wametakiwa kufuata kikamilifu miongozo, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, sambamba na kudumisha maadili na uadilifu wanapoanza kutekeleza majukumu yao.
Wito huo umetolewa leo, Novemba 21, 2025, na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, wakati akifungua mafunzo ya awali kwa watumishi hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Graphite, Makao Makuu ya Tume jijini Dodoma.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhandisi Lwamo amesisitiza umuhimu wa watumishi hao wapya kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuhatarisha uadilifu wao katika sekta ya madini.
“Sekta ya madini ina vishawishi vingi. Mara nyingi wafanyabiashara wanatafuta njia za kupata faida kubwa. Kwenye dhahabu kuna masuala ya ubora na usafi (quality na purity). Msikubali kushawishiwa kwa vijisenti ambavyo vinaweza kuwatia hasara baadaye,” amesema.
Ameongeza kuwa Tume haitavumilia aina yoyote ya mwenendo usio wa uadilifu:
“Epukeni tamaa za mafanikio ya haraka. Mmefundishwa maadili, myashike na myazingatie. Itanisikitisha sana kuona mtumishi akipoteza ajira kwa sababu ya kukiuka misingi ya uadilifu.”
Mbali na suala la maadili, Mhandisi Lwamo amewahimiza waajiriwa hao kuanza kupanga maisha yao ya baadaye, ikiwemo maandalizi ya kustaafu, akisema kutobweteka kutawasaidia kujenga mustakabali bora wa kazi na maisha.
Awali, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Nsajigwa Kabigi, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa wa muundo na majukumu ya Tume ya Madini, haki na wajibu wa mtumishi wa umma, taratibu za ukaguzi na uhifadhi mazingira migodini, haki madini, pamoja na sheria na kanuni mbalimbali zinazosimamia sekta ya madini.
“Mafunzo mliyopata yawafanye kuwa mabalozi wazuri wa Tume. Wengi wenu mtakwenda kwenye ofisi za Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs). Nidhamu iwe nguzo na muende mkaiwakilishe Tume kwa weledi,” amesema.
Kwa niaba ya waajiriwa wenzake, Dorcas Michael ameushukuru uongozi wa Tume ya Madini kwa kuwapokea na kuwapa ajira, huku akiahidi kwamba watatekeleza kwa vitendo yote waliyofundishwa na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.








