NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
WARSHA ya mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kidijitali – Tanzania Chamber Portal imezinduliwa rasmi jijini Arusha, ikiwa ni hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya teknolojia ndani ya Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).
Akizungumza wakati wa ufunguzi kwa niaba ya Rais wa TCCIA, Mwenyekiti wa TCCIA Arusha, Walter Maeda, amesema mfumo huu mpya utaongeza uwazi, ufanisi na kasi ya utoaji huduma kwa wanachama wa chemba hiyo na Wafanyabiashara nchi nzima.
Warsha hiyo ya siku nne imewakutanisha washiriki kutoka Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, ambapo wanajengewa uwezo wa kutumia mfumo huo kwa usahihi kupitia timu ya wataalamu wa TCCIA kwa kupitia ufadhili wa Trademark Africa(TMA).
Kwa mujibu wa Ofisa TEHAMA wa TCCIA, Florian Mihyo, mafunzo haya yanafanyika kikanda ili kuhakikisha kila kanda inajengewa uelewa wa kutosha kabla ya uzinduzi rasmi.
Mfumo huo utawezesha wanachama na wafanyabiashara wote kwa ujumla kupata kwa urahisi huduma kama usajili, cheti cha uanachama, Cheti cha Uasili wa Bidhaa,Uwasilishaji wa Viwazo visivyo vya Kiforodha kwa wafanyabiashara wanapeleka bidhaa nje ya Nchi lakini pamoja na dawati la huduma kwa wateja mtandaoni.
Washiriki wamepongeza hatua hiyo, wakisema itarahisisha biashara na kupunguza urasimu.
Frida Shedafa, Ofisa Forodha II – TRA Namanga mkoa wa Arusha, amesema mfumo huo “utaimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma na Sekta binafsi, kupunguza urasimu na kuongeza uwazi, hasa kwenye maeneo ya mpakani kama Namanga.”
Warsha hizi zinatarajiwa kuharakisha matumizi ya teknolojia ndani ya TCCIA na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa taifa.



