NA MWANDISHI WETU, MARA
MKOA wa Mara umeweka rekodi mpya katika uzalishaji wa madini baada ya kuzalisha dhahabu yenye uzito wa tani 67.41, ikiwa na thamani ya Sh. Trilioni 8.881 katika kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2021 hadi Oktoba 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Ofisa Mazingira, Byalugaba Chakupewa, hivi karibuni alisema mauzo ya dhahabu hiyo yamechangia mapato ya Serikali zaidi ya Sh.Bilioni 605.86 kupitia mrabaha, ada za ukaguzi na tozo mbalimbali.
Aidha, Chakupewa alisema kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini mkoani Mara imekusanya maduhuli ya Sh.Bilioni 78.7 katika robo ya kwanza ya mwaka, sawa na asilimia 37.48 ya lengo la mwaka la Sh.Bilioni 210.3.
Kwa mujibu wake, ofisi hiyo pia imetoa leseni 2,478 za shughuli za madini, hatua iliyosaidia kuongeza ajira, kuchochea uwekezaji na kuimarisha mapato ya halmashauri.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo yanatokana na usimamizi madhubuti wa sekta hiyo na mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo yameufanya Mkoa wa Mara kuendelea kuwa miongoni mwa vinara wa uzalishaji wa madini nchini.





