NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
ZAIDI ya watu milioni nne waishio katika Mkoa wa Dar es Salaam wanatarajiwa kupiga kura Oktoba 29,2025 katika Uchaguzi Mkuu wa Madiwani,Wabunge na Rais, huku maandalizi yote yakiwa yamekamilika kwa mafanikio makubwa.

Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 27,2025 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu, akisisitiza umuhimu wa kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowaona wanafaa.

“Huu ni wakati wa kufanya maamuzi ya busara kwa kuchagua viongozi mnaowaamini. Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kila kitu kinaenda kwa utulivu na uwazi,” amesema Chalamila
Ameeleza kuwa hali ya usalama katika jiji hilo imeimarika na hakuna dalili za vurugu, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiwa katika maeneo yote
kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.
Chalamila pia amewataka viongozi wa serikali za mitaa kuhakikisha usalama wa miundombinu muhimu ikiwemo ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) pamoja na barabara, ili kuepusha uharibifu wowote.

Aidha, ametoa onyo kwa watu au makundi yatakayojaribu kuhamasisha maandamano au vitendo vya uchochezi wakati wa uchaguzi, akisema serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Amehitimisha kwa kuwataka wakazi wa Dar es Salaam kudumisha amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa uchaguzi ni fursa ya kidemokrasia inayopaswa kuenziwa kwa utulivu na heshima kwa maamuzi ya wengi.

