
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WANAFUNZI 10 wa kike nchini wamepata ufadhili wa masomo katika masuala
ya Nishati Endelevu kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) na Ubalozi wa Ireland katika mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwa ni
matokeo ya ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Nishati na UNDP katika
kuwajengea uwezo Wanawake wa Tanzania katika masuala ya Nishati.
Kutolewa kwa ufadhili huo ni utekelezaji wa Mpango Kazi wa mwaka 2018
wa Matumizi Bora ya Nishati ambapo pamoja na masuala mengine, suala la
kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya nishati limeainishwa.
Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza Wanafunzi hao jijini Dar es
Salaam leo Ijumaa Oktoba 24, 2025, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Ziana
Mlawa amesema kuwa kutolewa kwa ufadhili huo kunawawezesha Wanawake wa
Tanzania kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mfumo wa nishati
endelevu na rafiki kwa mazingira huku kukiwa na kiwango kidogo cha
uzalishaji wa hewa ukaa.
Mlawa ameeleza kuwa, Serikali, kupitia Wizara ya Nishati, imeendelea
kuwawezesha wanawake katika masomo ya nishati, hususan katika ngazi ya
elimu ya juu.
Vilevile, kupitia ushirikiano na wadau wake mbalimbali wakiwemo
Ubalozi wa Ireland na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP),
imeendelea kuweka kipaumbele katika uwekezaji wa upatikanaji wa elimu
ya juu na masuala ya uongozi kwa wanawake.
Ameongeza kuwa, tangu kuanza kutolewa kwa ufadhili wa masomo katika
sekta ya Nishati kupitia Mpango Kazi wa mwaka 2018 wa Matumizi Bora ya
Nishati wanafunzi wa kike takriban 35 wamenufaika na ufadhili wa
masomo katika mwaka 2023/2024 na 2024/2025.
Mlawa ameishukuru UNDP na Ubalozi wa Ireland kwa kutoa ufadhili huo
wa masomo ambao mwaka huu unafikia ukomo wake huku akiwaomba kuendelea
kutoa ufadhili wa masomo hayo ambayo ni muhimu katika ukuaji wa Sekta
ya Nishati.
Pia amekishukuru Chuo cha DIT ambacho ndicho kitatoa mafunzo kwa
wanafunzi waliofadhiliwa.
Mlawa pia amewapongeza Wanafunzi wa kike waliopata ufadhili akiahidi
kuwa Wizara iko tayari kushirikiana nao, kuwasaidia na kuwapatia
majukwaa ambapo mawazo yao na ubunifu wao utasikika na kuthaminiwa.

