NA MWANDISHI WETU, PWANI
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeanza utekelezaji wa mpango wa kuendeleza maeneo yake katika Mkoa wa Pwani kwa kujenga majengo ya ghorofa, hatua inayolenga kuongeza fursa za uwekezaji na kuchochea maendeleo ya makazi ya kisasa katika mkoa huo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa TBA, Said Mndeme, alisema kuwa, Taasisi yetu imeanza kuchukua hatua za kulinda na kuendeleza maeneo yake kwa kuweka alama za utambulisho na nyaraka halali za umiliki ili kuepusha uvamizi na matumizi yasiyo sahihi.

Mndeme alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa TBA wa kuhakikisha ardhi ya serikali inatumika kwa tija zaidi kiuchumi, ikiwemo kuanzisha miradi ya kimkakati ya makazi na biashara kulingana na mahitaji ya soko la sasa.
Ameeleza kuwa tayari taasisi hiyo imeanza mchakato wa maandalizi ya miradi mbalimbali, ikiwemo eneo la Mwendapole lenye zaidi ya hekari 92, ambalo limeanza kukaguliwa kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya kisasa yatakayoongeza thamani ya ardhi na mapato kwa serikali.



Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, amepongeza juhudi za TBA akisema, Serikali inaunga mkono utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuwa inalenga kuboresha mandhari ya mkoa na kutoa fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya ujenzi.

Amesema, Ujenzi wa majengo ya juu ni hatua muhimu ya kuvutia wawekezaji wapya, kukuza shughuli za kiuchumi, na kuongeza thamani ya maeneo yanayozunguka viwanda vinavyokua kwa kasi katika Mkoa wa Pwani.
Aidha, Kunenge ameagiza TBA kuhakikisha miradi yote ya ujenzi inazingatia ubora, usalama na viwango vya kitaifa ili kuwezesha upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi na watumishi wa umma.
Amesisitiza kuwa, Miradi hiyo ni fursa ya kiuchumi itakayochangia kuongeza mapato ya serikali, ajira kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla.

