NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SERIKALI imezindua rasmi utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimataifa wa mazingira ujulikanao kama “Mbinu Chanya na Jumuishi za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Kulinda Bayoanuai” (Integrated Net-Zero Nature-Positive Solutions for Climate and Biodiversity Protection), unaolenga kuendeleza sekta ya misitu kwa lengo la kuinua maisha ya watu.
Akizungumza leo Oktoba 23,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha Kamati ya Usimamizi wa Mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, ambaye ni Mwenyekiti alisema mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 38 ni uthibitisho wa kuaminiwa kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Mradi huu ni ushahidi wa juhudi za Serikali katika kulinda mazingira, kuhifadhi misitu na kuhamasisha nishati safi. Dunia inatambua uongozi wa Tanzania katika masuala ya uchumi wa kijani ndio maana baadhi ya wadau wa Mradi huu pamoja na Serikali yenyewe ni Mfuko wa Dunia wa Mazingira na wenzetu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ,” amesema Dk. Abbasi.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Wizara ya Fedha, Tume ya Mipango, UNDP, na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF).
Naye Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini ambaye ni Mwenyekiti Mwenza katika usimamizi wa mradi huo,Shigeki Komatsubara, ameahidi kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kuendeleza miradi inayolinda mazingira lakini na kuinua maisha na utu wa watu.