NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imewahimiza wafanyabiashara, wakulima na wamiliki wa viwanda nchini kutumia kikamilifu fursa za kibiashara zinazotokana na kuimarika kwa diplomasia ya uchumi kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatano Oktoba 22,2025 katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahamoud Thabit Kombo (MP), amesema serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na chemba hiyo ili kuwezesha maendeleo ya sekta binafsi kupitia uhusiano mzuri wa kimataifa unaochochea fursa mpya za kiuchumi.

“Tutaendelea kufanya kazi na TCCIA katika kuhakikisha wakulima, wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda wanainufaika na fursa zinazoibuka kutokana na diplomasia ya uchumi na uhusiano wetu na mataifa ya nje,” amesema Balozi Kombo.

Kwa upande wake, Rais wa TCCIA,Vicent Minja, alisema mkutano huo wa mwaka umejikita katika mchakato wa kuifanyia marekebisho katiba ya chemba hiyo ili iendane na mahitaji ya sasa.

Amesisitiza umuhimu wa kuwajumuisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika mifumo ya uongozi na maamuzi ya TCCIA.
Pia aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na taifa la Iran kutokana na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za uchumi.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk. Godwill Wanga, aliwataka wafanyabiashara nchini kuongeza mshikamano na ushirikiano katika kukuza sekta ya biashara, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kidijitali kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mkutano huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi na za umma, ikiwa ni jukwaa la kujadili changamoto na fursa za kibiashara ndani na nje ya nchi.


