NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa mvua za chini ya Wastani hadi wastani zinazotarajiwa katika maeneo mengi hapa nchini zinaweza zikasababisha upungufu wa unyevu wa udongo pamoja na kuathiri pia upatikanaji wa maji na malisho kwa mifugo.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Oktoba 17,2025 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a wakati ikitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya mwelekeo wa mvua za msimu kwa kipindi cha Novemba 2025 hadi Aprili, 2026.
Dk. Chang’a amesema kwa upande wa kanda ya Magharibi ambayo inajumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora inatarajiwa kupata mvua hizo za chini ya wastani hadi wastani ambazo zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu na ya nne mwezi Oktoba mwaka huu na kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili 2026, huku upande wa kanda ya kati ambayo inajumuisha mikoa ya Singida na Dodoma inatarajiwa pia kupata pia mvua za chini ya wastani hadi wastani.
Amesema kwa upande wa kanda ya nyanda za juu kusini magharibi ambayo inajumuisha mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa na Morogoro inatarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinazotarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2025 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2026.
“Kwa upande wa Pwani ya kusini na maeneo ya kusini mwa nchi inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, mvua zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi Chini ya Wastani katika mikoa hiyo na zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Desemba, 2025 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili na ya kwanza ya mwezi Mei, 2026,” amesema
Dk. Chang’a amesema kufuatia uwepo wa mvua hizo kutasababisha athari hiyo ya upungufu wa unyevu wa udongo jambo ambalo linaweza kuathiri ukuaji na maendeleo ya mazao na kupunguza mavuno hususani kwa mazao yanayategemea mvua na kwamba kuna uwezekano wa kuongezeka kwa wadudu waharibifu wa mazao kama vile panya na mchwa.
Amesema wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba kwa wakati, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa kuzingatia hali ya unyevu katika udongo. Aidha, wanashauriwa kutumia mbinu bora na teknolojia za kuhifadhi maji shambani.
“Vilevile, inashauriwa kuimarisha miundombinu ya kilimo na kudhibiti kwa wakati magonjwa ya mimea na wadudu waharibifu ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza. Wakulima wanashauriwa pia kutafuta taarifa sahihi kutoka kwa maafisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa msimu wa wilaya husika katika kuchagua mbegu na zao sahihi.
“Aidha, wakulima na Maofisa Ugani wanashauriwa kuendelea kutumia utabiri wa siku na wa siku kumi ili kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa utabiri wa msimu,” amesema .
Hata hivyo Dk. Chang’a amesema upungufu wa mvua unaotarajiwa katika maeneo mengi unaweza kuathiri pia upatikanaji huo wa maji na malisho kwa mifugo hali ambayo inaweza kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Amesema kufuatia hali hiyo wafugaji wanashauriwa kuweka na kutekeleza mipango bora ya matumizi na uhifadhi wa maji pamoja na vyakula vya mifugo.
Amesema wafugaji pia wanashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri unaotolewa na maofisa ugani ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza na kuendelea kunufaika na hali ya hewa inayotarajiwa wakati wa msimu.
Amesema katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani, hifadhi za taifa na mapori ya akiba yanatarajiwa kukumbwa na upungufu wa malisho na maji kwa wanyamapori hali ambayo inaweza kusababisha migogoro kati ya wanyamapori na jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Amesema wanyamapori wanaweza kuvamia makazi ya binadamu, hivyo kuongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa kwa mifugo na kwamba hali hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa binadamu na wanyama wa kufugwa kutokana na mashambulizi ya wanyama wakali.
“Mamlaka husika zinashauriwa kuboresha miundombinu mbalimbali katika mbuga na mapori ya akiba na kujenga uelewa kwa jamii ili kuchukua hatua stahiki kutokana na athari zinazoweza kujitokeza. Hivyo, jamii inashauriwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanyamapori wanapoingia katika maeneo yao ya makazi,” amesema
Vilevile Dk. Chang’a amesema sekta ya usafiri na usafirishaji inatarajiwa kunufaika kutokana na upungufu wa mvua katika msimu huu hata hivyo amesema uwezekano wa vipindi vifupi vya ongezeko la mvua vinaweza kuathiri au kusitisha shughuli kwa muda.
Amesema wadau wa sekta hiyo ya usafirishaji nchi kavu, majini na angani wanashauriwa kuchukua hatua stahiki katika utekelezaji wa ujenzi, ukarabati na matengenezo kinga ya miundombinu mbalimbali pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kupunguza au kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.
Amesisitiza kuwa kupungua kwa kina cha maji kwenye mabwawa na mtiririko wa maji kwenye mito kunaweza kutokea, hali ambayo inaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali na kusababisha migogoro kati ya watumiaji wakubwa na wadogo.
“Uzalishaji wa umeme kwa kutumia nguvu za maji unaweza kuathiriwa. Hata hivyo, ujenzi wa miradi mipya ya uzalishaji umeme pamoja na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi unaweza kunufaika na hali hii. Katika sekta ya madini, uzalishaji wa madini kwa wachimbaji wadogo unaweza kuongezeka kutokana na upungufu wa mvua ila shughuli za uchimbaji madini zinazotegemea maji kwa kiasi kikubwa zinaweza kuathirika,” amesema
Dk. Chang’a amesema upungufu wa upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, na mifugo unatarajiwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chini ya wastani hadi Wastani, hivyo mamlaka za Serikali za Mitaa zinashauriwa kuchukua hatua madhubuti ikiwemo kuimarisha na kuboresha mifumo ya usambazaji maji safi kwa matumizi ya nyumbani na Sekta nyingine muhimu.
Hata hivyo, amesema vipindi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo vinaweza kusababisha kutuama kwa maji na mafuriko hali hiyo inaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu na upotevu wa maisha na mali.
“Mamlaka za serikali za mitaa zinashauriwa kuboresha mifumo ya mifereji ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mafuriko sambamba na kutoa elimu kwa jamii juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika utekelezaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi,” amesema

